
Mtangazaji na mchekeshaji maarufu kutoka Kenya, Oga Obinna, ametoa ushauri kwa mabinti wadogo kuzingatia maisha yao binafsi na kujiepusha na kupata mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 26.
Kupitia ujumbe wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Obinna alisisitiza kuwa umri wa kati ya miaka 20 hadi 26 ni kipindi muhimu sana kwa wanawake kujijenga kifedha, kielimu na kimaendeleo, badala ya kuharakisha kuanzisha familia au kuhamia kwa wanaume.
“Huo ndio muda wenu wa ku-focus. Wakati wenu wa kujitengenezea maisha, siyo wa kulea watoto au kuhamia kwa wanaume,” alisema Obinna.
Obinna aliongeza kuwa wanawake wengi hujikuta wakijutia maamuzi ya mapema ya kuanzisha familia bila kuwa tayari kiakili na kifedha, jambo ambalo humzuia mwanamke kufikia malengo yake ya maisha.
Kauli yake imezua mijadala mitandaoni, huku baadhi wakiiunga mkono kama ujumbe wa kuhamasisha mabinti kupanga maisha yao kwa busara, ilhali wengine wakitafsiri kama mtazamo unaopuuza hali halisi ya maisha ya baadhi ya wanawake.
Oga Obinna amekuwa akijulikana kwa maoni yake yenye utata lakini pia yenye lengo la kuamsha fikra, hususan kwa vijana wanaofuatilia mitindo ya maisha, mahusiano na maendeleo binafsi.