LifeStyle

Otile Brown Asema Kifo cha Raila Kumfundisha Utu

Otile Brown Asema Kifo cha Raila Kumfundisha Utu

Mwanamuziki nyota wa R&B kutoka Kenya, Otile Brown, ameonyesha kuguswa kwa kina na kifo cha aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Amolo Odinga, akisema kimebadilisha mtazamo wake kuhusu maisha na maana halisi ya uongozi.

Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Otile Brown ameeleza kuwa kifo cha Raila kimemfanya kutafakari kuhusu maisha, akisema kimeonyesha wazi kwamba dunia ni kubwa kuliko mwanadamu na kwamba hatuna mamlaka ya kudumu ndani yake.

Msanii huyo amesema tukio hilo limemnyenyekeza sana na kumfanya kutambua thamani ya kuwa na uongozi wenye misingi ya utu na upendo kwa watu. Ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kujifunza kutokana na maisha ya Raila Odinga, ambaye licha ya changamoto alizokumbana nazo, aliendelea kujitolea kujenga jamii bora.

Kwa mujibu wa Otile, kiongozi mzuri ni yule anayejenga jamii imara na anayeacha alama nzuri hata baada ya kuondoka. Amesisitiza kuwa pesa pekee haitoshi kujenga kizazi bora katika jamii iliyovurugika kimaadili, akieleza kuwa mali haina maana ikiwa mtu hana moyo wa kuridhika na kufanya mema.

Hata hivyo, Otile Brown, amehitimisha ujumbe wake, akiwataka Wakenya kuendelea kupendana na kujenga taifa lao kwa umoja na moyo wa uzalendo, akisema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha nchi inaendelea kuwa mahali bora kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *