Rapa kutoka nchini Tanzania, Rose Ree, ameelezea huzuni yake kufuatia machafuko yanayoripotiwa kutokea nchini humo baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata mkubwa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo ameandika ujumbe mzito akionesha masikitiko yake kwa hali ilivyo nchini Tanzania, akisema kwamba moyo wake unaumia kutokana na machafuko hayo na kwamba bado analipenda taifa lake kwa moyo wote.
Msanii huyo ameongeza kuwa giza kuu hutanda karibu na mapambazuko, akimaanisha kwamba kuna matumaini ya siku mpya kuwadia kwa Watanzania, kabla ya kumalizia kwa kusema Mungu aibariki Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa, maandamano bado yanaendelea katika maeneo kadhaa nchini Tanzania, huku wananchi wakipinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa, ambayo ilimtangaza mgombea wa chama tawala Samia Suluhu Hassan kuwa rais mteule.
Uchaguzi huo umekumbwa na pingamizi kubwa kutoka kwa wananchi na vyama vya upinzani, hali iliyosababisha baadhi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kusitisha shughuli zao kutokana na sababu za kiusalama.