Msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny, ametoa onyo kali kwa mtu anayejifanya yeye kwenye ukurasa wa Facebook ulioidhinishwa (verified), wenye wafuasi zaidi ya milioni 3.4, baada ya akaunti hiyo feki kutumia jina lake kuposti picha na video za matukio ya kusikitisha yanayoendelea nchini Tanzania.
Kupitia instastory zake, Rayvanny alionekana mwenye hasira akimtahadharisha mtu huyo kuacha mara moja kutumia jina na taswira yake kwa njia za udanganyifu.
Rayvanny amewataka mashabiki wake kuwa makini na kuripoti ukurasa huo kwa mamlaka husika za mtandao wa Facebook, akisisitiza kuwa yeye hana uhusiano wowote na maudhui hayo yanayosambazwa.
Akaunti hiyo feki inadaiwa imekuwa ikichapisha maudhui yanayohusiana na matukio ya vifo, ikiwemo picha za miili ya watu waliopoteza maisha kwenye maandamano ya kupinga uchaguzi uliokamilika nchini Tanzania, jambo ambalo limezua taharuki miongoni mwa mashabiki na wafuasi wa msanii huyo.