Mwanamuziki kutoka Uganda, Sheebah Karungi, amewajibu kwa msimamo thabiti wakosoaji wanaopinga mtindo wake wa mavazi unaoonyesha maungo ya mwili wake.
Sheebah, amesema hana mpango wa kuomba msamaha kwa jinsi anavyojivalisha, akisisitiza kuwa amewekeza sana katika mwili wake kwa kufanya mazoezi na kutumia pesa zake, hivyo anaamini ana haki ya kuonyesha matokeo ya kazi yake kwa njia anayoona inafaa bila kudhibitiwa na yeyote.
Mwanamuziki huyo, ambaye mara kwa mara amekuwa akitumia jukwaa lake kuhamasisha wanawake juu ya kujikubali na kujiamini, amesisitiza kuwa hana sababu ya kujificha au kubadilisha mtindo wake wa maisha kwa sababu ya maoni ya watu, akisema anajivunia kuwa mwanamke huru anayejiamini.
Hata hivyo, Sheebah, amesema ataendelea kuvaa na kuishi kwa namna inayompa furaha bila kuzingatia vigezo vya kijamii vinavyomlazimisha kubadilika.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya mwanamuziki huyo kuchapisha picha kadhaa mitandaoni ambazo, kwa mujibu wa wakosoaji, zinaonyesha sehemu kubwa ya maumbile yake, jambo ambalo wamedai halimpendezi kama mzazi.