
Msanii maarufu wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Octopizzo, ameibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha ujumbe mzito katika mtandao wa X (zamani Twitter), akiwataka Wakenya wawe makini na hali ya kisiasa nchini.
Kupitia ujumbe huo, Octopizzo amewataka raia kukataa kile alichokiita usahaulifu wa kisiasa, akieleza kuwa upinzani unaojitokeza hivi sasa si mpya kwa kweli, bali unaundwa na viongozi waliowahi kushika nyadhifa serikalini kwa muda mrefu bila kuleta maendeleo ya maana kwa taifa.
“Wakenya hawapaswi kusahau historia ya kisiasa. Huu unaoitwa upinzani mpya ni mkusanyiko wa viongozi waliokataliwa, au waliodumu serikalini kwa zaidi ya miaka ishirini bila kuwa na mafanikio yoyote ya kushikika. Wanaonekana kutamani madaraka, si mageuzi ya kweli,” ameandika msanii huyo.
Octopizzo ameendelea kwa kutoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kutanguliza maendeleo ya taifa badala ya kushabikia watu binafsi au vyama.
“Tuwe waangalifu na tujitolee kwa maendeleo, si kwa kushabikia watu au majina. Kama taifa, tunastahili uongozi unaowajali wananchi si wakati wa uchaguzi pekee, bali kila siku.” Ameongeza kwa msisitizo.
Ujumbe huu umepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni, baadhi ya wananchi wakimsifu kwa kutoa kauli yenye busara na ujasiri,huku wengine wakitumia fursa hiyo kujiuliza maswali kuhusu mwelekeo wa kisiasa nchini.
Hii si mara ya kwanza kwa Octopizzo kutoa maoni kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa, kwani amekuwa akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kuhamasisha umma kuhusu haki, uwajibikaji, na maendeleo ya vijana nchini.