
Msanii wa reggae kutoka Jamaica, Sizzla Kalonji, amekanusha vikali madai kuwa alijiondoa kwenye tamasha la One Caribbean Music Festival nchini Trinidad kwa sababu ya kutaka kulipwa sawa na Vybz Kartel. Kupitia taarifa rasmi kwa jina lake halisi, Miguel Collins, Sizzla amesema madai hayo ni uongo na hayana msingi.
Sizzla ameeleza kuwa yeye na timu yake walikubali kushiriki kwenye tamasha hilo kwa mkataba wa malipo ya awali ya asilimia 50, lakini hadi siku ya onyesho walikuwa wamelipwa asilimia 10 pekee. Alidai kuwa alipendekeza walipwe kiwango kilekile kilichokuwa kimetengwa kwa msanii kinara ambaye hakufika, ili yeye achukue nafasi hiyo na kusaidia kuendeleza tamasha.
Licha ya hali hiyo, Sizzla aliwasifu waandaaji na wadhamini kwa jitihada zao, akisema walifanya kazi nzuri ila kilichoharibu mambo ni kutokuwepo kwa msanii mkuu. Aidha, alitumia muda wake Trinidad kufanya kazi na wanamuziki wa huko na kueleza kuwa bado anaipenda nchi hiyo.
Hadi sasa, waandaaji wa One Caribbean Music Festival bado hawajatoa majibu rasmi kuhusu madai ya Sizzla, huku mashabiki wakitaka uwazi na uwajibikaji kwa ajili ya matamasha yajayo
Tamasha la One Caribbean Music Festival lililokuwa limetangazwa kuwa na wasanii wa kimataifa, limekumbwa na changamoto kadhaa kufuatia kujiondoa kwa baadhi ya mastaa waliokuwa wakitarajiwa kutumbuiza, hali ambayo imeibua maswali miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani katika kanda hiyo