Kampuni kubwa za teknolojia duniani, Sony na TCL, zimetangaza kuingia katika ushirikiano rasmi kwenye biashara ya televisheni na vifaa vya burudani vya nyumbani, ikiwemo speakers, home theaters na mifumo ya sauti.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, TCL itakuwa na umiliki mkubwa wa hisa katika ushirikiano huo kwa asilimia 51, hatua inayoiweka kampuni hiyo ya China kama mdau mkuu katika biashara hiyo. Sony, kwa upande wake, itaendelea kubaki kama mshirika muhimu, huku chapa maarufu ya BRAVIA TV ikiendelea kuwepo sokoni chini ya ushirikiano huo mpya.
Hatua hiyo inatajwa kuwa habari kubwa kwa TCL, kwani inaipa nafasi ya kuimarisha ushawishi wake katika soko la kimataifa la televisheni kwa kushirikiana na moja ya chapa kongwe na zenye heshima kubwa duniani.
Katika mgawanyo wa majukumu, Sony itachangia teknolojia yake ya ubora wa picha, mifumo ya sauti na nguvu ya brand yake, huku TCL ikichukua jukumu kubwa katika uzalishaji na maendeleo ya teknolojia ya display za TV, eneo ambalo imekuwa ikifanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni.