Entertainment

Spice Diana Mbio Kuwabariki Mashabiki na Albamu Mpya

Spice Diana Mbio Kuwabariki Mashabiki na Albamu Mpya

Msanii nyota wa muziki wa Uganda, Spice Diana, ameweka wazi kuwa yuko mbioni kukamilisha albamu yake ya kwanza ya studio, akiahidi mashabiki wake kuwa itazinduliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Spice Diana, ambaye amekuwa kwenye tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka kumi, amesema huu ndio mradi wake mkubwa zaidi, na anaamini utakuwa wa kipekee kuliko kazi zake zote za awali. Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda, msanii huyo alieleza kuwa albamu hiyo ina nyimbo nyingi, lakini sasa anapitia changamoto ya kuchagua ni zipi ataweka rasmi kwenye albamu hiyo.

Β β€œNafanya kazi ya albamu. Kuna nyimbo nyingi sana hadi napata shida kuchagua. Lakini nitahakikisha albamu itatoka kabla ya mwaka kuisha. Ni kazi bora kabisa kutoka kwangu kwa sababu nimewekeza muda na nguvu nyingi,” alisema Spice Diana.

Albamu hiyo inakuja katika kipindi ambacho wasanii wengi wa Uganda wameanza kuelekeza nguvu zao kwenye utayarishaji wa albamu kamili, tofauti na zamani ambapo walikuwa wakizingatia zaidi nyimbo za mtu mmoja mmoja.

Spice Diana ataungana na orodha ya wasanii wengine wa Uganda waliokwisha toa albamu, akiwemo Sheebah, Juliana Kanyomozi, Azawi, Bebe Cool, Eddy Kenzo, Navio, A Pass na wengine.

Mashabiki wake wanaisubiri kwa hamu kazi hiyo mpya, ambayo inatarajiwa kuonyesha ubunifu na mwelekeo mpya katika muziki wa Spice Diana.