Msanii wa rap nchini Kenya, Stevo Simple Boy, ameongeza hatua kubwa kwenye kazi yake baada ya kusaini dili la ubalozi na kampuni ya usafiri na utalii, Skywide Tours and Travel.
Kampuni hiyo imemteua Stevo kama balozi wake mkuu, hatua ambayo inalenga kuvutia vijana na mashabiki wa muziki wake katika kutumia huduma zao za usafiri na utalii.
Uteuzi huu unatajwa kuwa ni fursa kubwa kwa msanii huyo, kwani unamfungulia milango mipya ya ushawishi kibiashara na kuongeza thamani yake nje ya muziki. Vilevile, unasaidia katika kukuza chapa ya Skywide Tours and Travel kwa kushirikiana na jina linalopendwa na vijana wengi nchini.
Dili hili linamweka Stevo Simple Boy kwenye nafasi ya kipekee ambapo muziki wake, uhalisia wa maisha yake, na mvuto wake kwa mashabiki vinatumika kama nyenzo ya kutangaza huduma za utalii na usafiri, huku likionekana kama hatua muhimu katika safari yake ya kukuza kipato na ushawishi.