
Rapper maarufu Stpd Boy ameibuka hadharani kuomba msamaha kwa mchekeshaji Oga Obinna, siku chache baada ya mvutano kati yao uliotikisa mitandao ya kijamii.
Kupitia Instagram, Stpd Boy alionekana mwenye majuto makubwa huku akikiri kwamba amerejea kwenye ulevi na maisha yasiyo na mwelekeo. Katika ujumbe wake, aliomba arudishwe kwenye kituo cha rehab ili aweze kuendelea na safari ya kupona na kurekebisha maisha yake.
“Nimeanguka tena kwenye mtego wa pombe. Nimekosea. Naomba Obinna anisamehe na anisaidie nirudi rehab. Sitaki kurudi kule nilikotoka,” alisema kwa hisia.
Kauli hii imekuja baada ya msanii huyo hapo awali kumkashifu Oga Obinna, akidai kwamba alimtumia kwa ajili ya umaarufu wakati alipompeleka rehab kwa mara ya kwanza. Madai hayo yalizua mjadala mkali mtandaoni, huku baadhi ya watu wakimtuhumu Stpd Boy kwa kutoonyesha shukrani.
Hata hivyo, kupitia video hii mpya, Stpd Boy ameonyesha kubadilika na kutambua mchango wa Obinna katika maisha yake, akisisitiza kuwa hana budi kuomba msaada tena ili aweze kujinasua kutoka kwenye mtego wa uraibu.
Mpaka sasa, Oga Obinna bado hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu msamaha huo wala ombi la kurejeshwa rehab.