
Mwanasiasa ambaye pia ni msanii wa hip hop, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, amewatolea uvivu mastaa wa muziki Diamond Platnumz, Ommy Dimpoz, Jux na Marioo kwa kauli zao za kuwataka wananchi kuacha kulalamikia Serikali na badala yake wafanye kazi.
Sugu, ambaye kwa sasa ni mwanachama wa chama cha upinzani nchini Tanzania, alicharuka mitandaoni akiwataka wasanii hao kuacha kudharau wale wanaopigania haki na badala yake kujiunga katika harakati za kudai mabadiliko ya kisiasa na kijamii.
Kupitia Instagram, amedai kuwa baadhi ya wasanii waliofanikiwa kimaisha wameanza kuwasihi wananchi “kutafuta kazi” badala ya kulalamika kuhusu changamoto zinazotokana na serikali. Kauli hizo, kwa mujibu wa SUGU, zinaonyesha dharau kwa wafuasi wa mageuzi.
Akitumia maneno makali, SUGU amesisitiza kuwa yeye na kizazi chake wamekuwa wakipiga muziki na kujipatia mamilioni tangu miaka ya 1998, lakini bado wamekuwa mstari wa mbele kudai haki na ustawi wa taifa. Ameongeza kuwa mafanikio binafsi hayapaswi kuzuia mtu kushiriki katika mapambano ya kijamii na kisiasa.