
Klabu ya Sunderland, ambayo imepanda daraja na itashiriki Ligi Kuu ya England (EPL) msimu ujao, imeanza mazungumzo rasmi na klabu ya Bayer Leverkusen kwa ajili ya kumsajili kiungo mkongwe Granit Xhaka.
Xhaka, ambaye aliwahi kuichezea Arsenal kwa mafanikio, kwa sasa ana umri wa miaka 32 na amebakisha miaka mitatu kwenye mkataba wake na Leverkusen. Hata hivyo, Sunderland imeonyesha nia ya dhati ya kumnasa kiungo huyo kwa kumtupia ofa ya mkataba wa miaka mitatu ya kuhudumu ndani ya klabu hiyo.
Uongozi wa Sunderland unaamini uzoefu wa Xhaka utakuwa muhimu kwa kikosi hicho kinachojipanga kushindana vikali kwenye EPL msimu ujao, huku wakitafuta kuongeza nguvu eneo la kiungo kwa wachezaji waliowahi kucheza kiwango cha juu barani Ulaya.
Mbali na Sunderland, taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya klabu kutoka Ligi Kuu ya Saudi Arabia pia zinaonyesha nia ya kumnasa Xhaka, ambapo endapo atasajiliwa, huenda akaungana tena na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Alexandre Lacazette, ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Neom nchini Saudi Arabia.