Bebe Cool Aomba Msaada wa Rais Kutangaza Albamu yake Mpya Kimataifa
Msanii maarufu wa Uganda na mwanzilishi wa Gagamel Crew, Bebe Cool, ametangaza kuwa albamu yake mpya “Break the Chains” itazinduliwa rasmi tarehe 30 mwezi huu. Albamu hiyo, ambayo ni ya saba katika kazi yake ya muziki, imechukua karibu mwaka mmoja kuikamilisha na imerekodiwa katika studio za kimataifa nchini Nigeria, Afrika Kusini, na Uingereza. Katika mahojiano na televisheni ya ndani, Bebe Cool alifichua kuwa hadi sasa ametumia zaidi ya shilingi bilioni 2.56 za Uganda katika utayarishaji wa albamu hiyo, ikijumuisha gharama za uandishi wa nyimbo, uzalishaji, mastering, na posho kwa timu yake ya uzalishaji ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa sasa ni kuisambaza na kuitangaza kimataifa, jambo ambalo litahitaji zaidi ya shilingi bilioni 7 (takriban dola milioni 2). “Mpaka sasa nimetumia dola 700,000. Kufanya muziki wa kiwango cha juu kunahitaji uwekezaji mkubwa. Ili niweze kuitangaza albamu hii kimataifa, nitahitaji zaidi ya dola milioni 2. Nampasa Rais Museveni kuniunga mkono katika hili,” alieleza Bebe Cool. Kwa msingi huo, Bebe Cool ameeleza kuwa anatafuta msaada wa kifedha kutoka kwa Rais Yoweri Kaguta Museveni, ili kufanikisha azma ya kuitangaza albamu hiyo katika soko la kimataifa. Anaamini “Break the Chains” itaweka muziki wa Uganda kwenye ramani ya dunia, na kuwa kichocheo kwa wasanii wengine kuwekeza katika kazi zao kwa maendeleo ya sekta nzima ya burudani nchini.
Read More