Msanii wa Uganda Alien Skin Adaiwa Kukamatwa kwa Tuhuma za Mauaji
Msanii mwenye utata kutoka Uganda, Alien Skin, ameripotiwa kuwekwa kizuizini baada ya kukamatwa mwishoni mwa juma kwa tuhuma za mauaji. Taarifa zinaeleza kuwa msanii huyo, ambaye ni bosi wa Fangone Forest, alinaswa na kikosi cha pamoja cha jeshi na polisi kilichozingira nyumba yake Jumamosi jioni. Inadaiwa kuwa katika upekuzi huo, maafisa wa usalama walikuta mapanga, upinde na mishale pamoja na silaha nyingine hatari nyumbani kwake, jambo lililoibua maswali zaidi kuhusu shughuli zake. Hata hivyo, vyombo vya usalama Uganda ikiwemo polisi na jeshi bado havijathibitisha rasmi kukamatwa kwake. Pamoja na hali hiyo, mashabiki wake wameanzisha kampeni mitandaoni wakitaka aachiliwe mara moja. Kwa mujibu wa mashabiki wake mitandaoni, kukamatwa kwake imehusishwa zaidi na kifo cha dansa mmoja maarufu wa Kampala ambaye alizikwa wiki iliyopita katika wilaya ya Mbale. Mashabiki wake wanadai msanii huyo ametupiwa lawama bila ushahidi wa moja kwa moja. Wakati huohuo, watumiaji kadhaa wa mitandao wamedai kuwa taarifa za kukamatwa kwake si za kweli, wakisisitiza kuwa Alien Skin yupo mafichoni na hajawahi kutiwa mbaroni. Madai ya kukamatwa kwa Alien Skin yameibuka saa chache tu baada ya Naibu Waziri wa Vijana nchini humo kuonya kuwa wasanii wanaoshirikiana na magenge ya kihalifu wako chini ya uchunguzi kwa makosa mbalimbali ikiwemo mauaji.
Read More