Amazon Yasitisha Ajira Mpya, AI Kuchukua Nafasi za Binadamu
Kampuni kubwa ya biashara mtandaoni duniani, Amazon, imetangaza mpango wa kupunguza baadhi ya nafasi za ajira kwa wafanyakazi wa maofisini (white-collar jobs), huku ikiendelea kuwekeza kwa kasi katika teknolojia ya akili bandia (AI) ili kuongeza ufanisi wa kazi. Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Amazon, Andy Jassy, kupitia waraka wa ndani kwa wafanyakazi. Alieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya Generative AI yanabadilisha kwa kasi jinsi kazi zinavyotekelezwa ndani ya kampuni hiyo, jambo linalopelekea kupungua kwa hitaji la wafanyakazi katika baadhi ya majukumu. “Kadri tunavyotumia zaidi teknolojia za AI na mawakala wa dijitali, tutahitaji watu wachache kutekeleza baadhi ya majukumu ambayo hapo awali yalihitaji wafanyakazi wa kawaida,” alisema Jassy. Hata hivyo, Jassy amewahimiza wafanyakazi wa Amazon kujiandaa na mabadiliko kwa kujifunza teknolojia ya AI ili kubaki na nafasi katika soko la ajira linalobadilika haraka. “Wale watakaokumbatia mabadiliko haya, kujifunza AI, na kuitumia kwenye kazi zao, ndio watakaonufaika zaidi katika zama hizi mpya,” aliongeza. Amazon tayari imechukua hatua ya kusitisha ajira mpya katika baadhi ya vitengo, hasa katika idara ya rejareja, sambamba na uwekezaji mkubwa wa zaidi ya dola bilioni 100 kwenye AI na miundombinu ya data centers. Hatua ya Amazon kuhamia kwenye AI inaakisi mwelekeo wa kampuni nyingine kubwa duniani kama IBM, Meta, na JPMorgan, ambazo pia zimeanza kutumia AI kwa lengo la kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.
Read More