Ibraah Atangaza Kuondoka Rasmi Konde Gang Baada ya Kikao na BASATA

Ibraah Atangaza Kuondoka Rasmi Konde Gang Baada ya Kikao na BASATA

Msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Abdallah maarufu kama Ibraah, ametangaza rasmi kuondoka kwenye lebo ya Konde Music Worldwide baada ya kikao cha mwisho kilichowahusisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na uongozi wa lebo hiyo. Kupitia mahojiano baada ya kikao hicho, Ibraah amethibitisha kuwa wamefikia mwafaka wa kumaliza tofauti zao na uongozi wa Konde Gang. Hata hivyo, ameeleza kuwa bado hajakabidhiwa baadhi ya vitu muhimu vinavyohusiana na kazi yake ya muziki, ikiwemo akaunti zake za digital platforms kama YouTube, Boomplay, na Spotify. Kwa upande wao, uongozi wa Konde Gang kupitia Sandra, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa lebo hiyo, wamethibitisha kuwa Ibraah atakabidhiwa rasmi akaunti hizo kabla ya mwisho wa leo. Aidha, Sandra amemtakia kila la heri Ibraah katika safari yake mpya ya muziki nje ya Konde Gang, akisisitiza kuwa hakuna uadui kati yao bali ni mabadiliko ya kawaida katika tasnia ya sanaa. Kuondoka kwa Ibraah kunakuja baada ya muda mrefu wa tetesi na hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake ndani ya Konde Gang. Mashabiki wake sasa wanangoja kwa hamu kuona ni wapi atapeleka kipaji chake na iwapo ataendelea kung’ara kama msanii huru. Hii ni miongoni mwa migogoro ya kimikataba inayozidi kuibuka katika tasnia ya muziki Tanzania, huku mashirika kama BASATA yakihimiza mazungumzo ya kidiplomasia kama njia ya kutatua mizozo kati ya wasanii na lebo zao. Ibraah alikuwa msanii wa kwanza kusainiwa Konde Music mwaka 2020, na ametoa nyimbo kadhaa zilizotikisa chati za muziki Afrika Mashariki, kama vile One Night Stand, Nani, na Dharau akiwa chini ya lebo hiyo.

Read More
 Wema Sepetu Aitwa na Bodi ya Filamu Nchini Tanzania Kisa Mavazi

Wema Sepetu Aitwa na Bodi ya Filamu Nchini Tanzania Kisa Mavazi

Bodi ya Filamu Tanzania imemwita rasmi msanii maarufu wa filamu za Bongo, Wema Sepetu, kufika katika ofisi zao kwa ajili ya mahojiano kufuatia kusambaa kwa picha jongevu (video clips) mitandaoni ambazo zinadaiwa kukiuka maadili ya kazi za sanaa nchini. Katika taarifa iliyotolewa na bodi hiyo, imeelezwa kuwa video hizo zinamuonesha Wema akiwa amevaa mavazi yasiyo na staha, jambo ambalo limeibua mjadala mkubwa mitandaoni na kuibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa tasnia ya filamu na jamii kwa ujumla. Bodi hiyo imekumbusha wasanii wote Nchini Tanzania kuzingatia maadili, sheria na kanuni za uendeshaji wa kazi za sanaa, hasa katika enzi hizi ambapo maudhui huenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii. Wema Sepetu, ambaye ni mmoja wa waigizaji maarufu na wenye ushawishi mkubwa nchini humo, bado hajatoa kauli rasmi kuhusiana na wito huo wa Bodi. Hata hivyo, mashabiki wake wamekuwa wakitoa maoni tofauti, baadhi wakimtetea na wengine wakihitaji afuate misingi ya maadili ya kazi za sanaa.

Read More