Bien Aikosoa Vikali Hatua ya NACADA Kupiga Marufuku Wasanii Kutangaza Pombe
Msanii nyota wa Kenya na mwanachama wa kundi la Sauti Sol, Bien-Aimé Baraza, ameikosoa vikali Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) kwa pendekezo la kuzuia watu mashuhuri kushiriki kwenye matangazo ya bidhaa za pombe. Kupitia ujumbe mzito alioutuma kwenye ukurasa wake wa Instagram, Bien amesema hatua hiyo ni ya kinafiki na inadhuru moja kwa moja sekta ya sanaa, ubunifu na maudhui, inayotegemewa na maelfu ya vijana kwa ajira. “Hii ni unafiki. Mnajifanya kuwajali vijana huku mnaua ndoto zao. Mnashangaa kwa nini ukosefu wa ajira ni mkubwa? Mnaua kila nafasi tunayopata,” aliandika Bien. Bien amesisitiza kuwa badala ya kuweka marufuku inayowakandamiza vijana, serikali inapaswa kuja na sera bora zinazolinda afya ya umma bila kuathiri vipato vya watu wanaotegemea sekta hizo. “Je, sisi ndio nchi ya kwanza kuwa na matatizo kama haya? Mbona tuendelee kujifanya watakatifu kuliko wengine wakati hatutoi suluhisho mbadala?” aliongeza Bien kwa ukali. Kauli yake imezua mjadala mitandaoni, wengi wakimtetea na kuitaka serikali kuweka sera zenye kuzingatia uhalisia wa kiuchumi.
Read More