Taylor Swift Aandika Historia kwa Kurejesha Haki za Muziki Wake
Mwanamuziki maarufu wa Marekani, Taylor Swift, ametangaza rasmi kwamba amepata tena umiliki rasmi kazi zake za awali, hatua kubwa inayohitimisha miaka ya mapambano kuhusu haki ya umiliki wa kazi za wasanii. Kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mitandao yake ya kijamii, Taylor alieleza furaha yake baada ya kurejesha umiliki wa albamu zake sita za mwanzo, ambazo awali zilikuwa chini ya lebo ya Big Machine. Katika ujumbe wake kwa mashabiki, Swift aliwashukuru kwa uungwaji mkono waliompa katika kipindi chote cha changamoto. “Sasa ninamiliki muziki wangu. Asante kwa kusimama nami, safari hii haingekuwa na maana bila ninyi,” aliandika. Ameeleza kuwa hatua hii si tu ya kihistoria binafsi, bali ni mfano kwa wasanii wengine kuhusu umuhimu wa kumiliki kazi zao. “Hili ni jambo kubwa sana kwangu na kwa kila msanii anayepigania haki zake,” aliandika Taylor Taylor Swift sasa anamiliki kikamilifu albamu zake maarufu kama Fearless, Speak Now, Red, 1989, Taylor Swift (debut), na Reputation ambazo zilimjengea jina kubwa kimataifa. Wengi wa mashabiki wake wamesherehekea ushindi huu kama hatua ya haki na mafanikio dhidi ya mfumo wa muziki unaowanyima wasanii udhibiti wa kazi zao. Mnamo mwaka 2019, lebo ya muziki ya Big Machine iliuza katalogi yake ya muziki kwa meneja wa muziki Scooter Braun, ambaye baadaye aliuzia kampuni ya uwekezaji ya Shamrock Capital bila ridhaa wala ushiriki wa Swift. Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa kimataifa kuhusu haki za wasanii katika tasnia ya muziki, huku Taylor akichukua hatua ya kurekodi upya albamu zake ili kupata tena udhibiti wa kisheria.
Read More