CAF Yasifu Ubora wa Kiufundi Katika Michuano ya CHAN PAMOJA 2024

CAF Yasifu Ubora wa Kiufundi Katika Michuano ya CHAN PAMOJA 2024

Kundi la Utafiti wa Kiufundi la Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF TSG) limepongeza makala ya tisa ya mashindano ya Soka ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) PAMOJA 2024, yakilitaja kama moja ya matoleo yenye mvuto mkubwa wa kiufundi katika miaka ya hivi karibuni. Akizungumza na vyombo vya habari, mwanachama wa kundi hilo na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ethiopia, Abraham Mebratu, pamoja na Mark Fish, mchezaji wa zamani wa kimataifa kutoka Afrika Kusini, walifafanua kuwa michuano hiyo imeonyesha maendeleo makubwa kiufundi. Kwa mujibu wa Fish, kiwango cha ushambulizi katika mashindano haya kimeongezeka, hali iliyochangia idadi kubwa ya mabao. “Tofauti na miaka iliyopita, timu nyingi zimeonyesha ujasiri wa kushambulia, na hii imesababisha mabao mengi kupatikana,” alisema Fish. Viongozi hao wa CAF TSG pia walieleza kuwa michuano ya CHAN PAMOJA 2024 imeleta mikakati mipya ya ukufunzi, pamoja na vipaji vipya vilivyoibuka kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloashiria mustakabali mzuri wa soka la Afrika. Hadi kufikia sasa, jumla ya mabao 74 yamefungwa katika mechi 36, ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mechi. Mchezo kati ya Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati, uliomalizika kwa mabao 4-2, ndio umeonekana kuwa mechi ya kusisimua zaidi kwa idadi ya mabao, huku Sudan ikijivunia ushindi mkubwa zaidi wa mabao 4-0 dhidi ya Nigeria.

Read More