Morocco Kuvaana na Zambia Leo Katika Mechi Muhimu ya Kundi A – CHAN

Morocco Kuvaana na Zambia Leo Katika Mechi Muhimu ya Kundi A – CHAN

Washindi mara mbili wa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), Morocco, watakuwa na lengo la kurejea kwenye njia ya ushindi leo jioni watakapomenyana na Zambia katika mechi ya Kundi A itakayopigwa kwenye uwanja wa Nyayo, Nairobi. Atlas Lions walizindua kampeni yao kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Angola, lakini wakapoteza mchezo wa pili kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Kenya siku ya Jumapili. Kwa upande mwingine, Zambia bado inawinda ushindi wake wa kwanza, baada ya kupoteza mechi zake zote mbili dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Angola. Morocco, ambao wamelenga kufuzu kwa hatua ya robo fainali, wanahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini yao ya kuendelea kushiriki mashindano haya. Nayo Zambia, ambayo inaburuza mkia bila alama yoyote, inahitaji ushindi ili kuhuisha matumaini ya kusalia katika michuano hiyo. Katika mechi nyingine ya kundi hilo hilo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itachuana na Angola katika uwanja wa Kasarani kuanzia saa mbili usiku. Mchuano huu pia ni wa muhimu katika kuamua hatma ya timu zitakazofuzu kwa hatua inayofuata. Baada ya raundi tatu za michuano ya Kundi A, Kenya inaongoza kwa alama saba, ikifuatiwa na Angola yenye pointi nne. DRC iko nafasi ya tatu kwa pointi tatu, Morocco ya nne, huku Zambia ikiwa mkiani bila pointi yoyote.

Read More
 Mataifa ya Afrika Mashariki Kushirikiana Kiusalama kwa CHAN 2025

Mataifa ya Afrika Mashariki Kushirikiana Kiusalama kwa CHAN 2025

Mataifa ya Afrika Mashariki yameafikiana kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha usalama wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani ya Nchi (CHAN) yatakayofanyika mwezi ujao. Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alisema kuwa mashauriano ya kina tayari yanaendelea kati ya Kenya, Uganda, na Tanzania, mataifa matatu yatakayoandaa mashindano hayo kwa pamoja ili kuimarisha usalama hasa kwenye maeneo ya mipakani na kuhakikisha usafiri salama wa timu na mashabiki. Murkomen alisisitiza kuwa hatua madhubuti zimewekwa ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa utulivu na bila hitilafu. Alibainisha kuwa udhibiti wa umati wa watu umepewa kipaumbele kikuu, ikizingatiwa kuwa maelfu ya mashabiki, wakiwemo wageni kutoka mataifa jirani, wanatarajiwa kuhudhuria mechi mbalimbali. β€œKuna mifumo ya uangalizi ya kisasa inayowekwa katika viwanja vyote vitakavyotumika, pamoja na itifaki za dharura ili kuhakikisha usalama wa mashabiki na wachezaji,” alisema Murkomen. Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kuimarisha mshikamano wa kikanda, si tu kupitia michezo, bali pia kupitia ushirikiano wa kiusalama na maandalizi ya pamoja yanayoakisi uwezo wa Afrika Mashariki kuandaa mashindano ya kimataifa kwa mafanikio.

Read More
 Wizara ya Michezo Yatenga Milioni 300 kwa Maandalizi ya Kip Keino Classic

Wizara ya Michezo Yatenga Milioni 300 kwa Maandalizi ya Kip Keino Classic

Wizara ya Michezo imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya sita ya Kip Keino Classic, yatakayofanyika tarehe 31 Mei kwenye uwanja wa Ulinzi, Nairobi. Waziri wa Michezo Salim Mvurya amesema kuwa matayarisho katika uwanja huo yanaendelea kwa kasi na yatakamilika kufikia jumamosi hii, kabla ya mbio hizo kufanyika ndani ya siku 11 zijazo. Mwaka huu, mashindano hayo yamegawanywa katika kitengo cha kitaifa na kitengo kikuu cha kimataifa, yakitarajiwa kuvutia jumla ya wanariadha 189, wakiwemo 59 kutoka Kenya. Mashindano haya ya siku moja yamehamishwa kutoka uwanja wa Nyayo, unaofanyiwa ukarabati kwa maandalizi ya fainali za CHAN zitakazofanyika mwezi Agosti mwaka huu. Kip Keino Classic ni sehemu ya kalenda ya mashindano ya World Athletics Continental Tour Gold, na kwa mara nyingine yanatarajiwa kuangazia vipaji vya ndani na nje ya Kenya huku yakitangaza taifa hili kama kitovu cha riadha duniani.

Read More