Chebet Ronoh Akanusha Kupigwa, Asema Picha Imehaririwa
Mchekeshaji na mtangazaji maarufu wa Kenya, Chebet Ronoh, amevunja ukimya wake kufuatia madai kuwa alishambuliwa na mpenzi wa rafiki yake kutokana na ugomvi wa chakula. Tuhuma hizo zilichochewa na picha iliyosambaa mtandaoni ikimuonesha akiwa na alama za majeraha usoni, hali iliyowatia hofu mashabiki wake. Hata hivyo, Ronoh amekanusha vikali madai hayo, akisema kuwa picha hiyo imehaririwa na haina ukweli wowote. “Niko sawa, salama nyumbani. Tafadhali niwacheni. Hiyo picha imehaririwa,” aliandika kwenye chapisho lake. Madai hayo yalichukua mkondo mpya baada ya bloga Mark Christian kudai kuwa Ronoh alipigwa na marafiki zake baada ya kulalamika kuwa walikula chakula chake. Taarifa hiyo ilizua mjadala mkali mitandaoni huku baadhi ya watu wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika. Hata hivyo, Ronoh amekanusha kuwepo kwa tukio hilo la kushambuliwa, akisisitiza kuwa yuko katika hali nzuri kiafya na kiakili. “Watu mitandaoni ni wakatili. Hebu fikiria mtu anahariri picha na kusema umepigwa ili apate kiki,” aliongeza katika ujumbe mwingine. Wafuasi wake wengi walipokea kwa afueni taarifa zake, huku wakimtaka aendelee kujilinda dhidi ya uzushi wa mitandaoni. Wengine walihoji uhalali wa bloga na watu mashuhuri wanaosambaza habari zisizothibitishwa ambazo huweza kuathiri maisha ya mtu binafsi. Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa polisi kuhusu tukio hilo, na Ronoh ameeleza wazi kuwa hatatoa maelezo zaidi kuhusiana na madai hayo.
Read More