Vurugu za Mashabiki Zazua Taharuki Katika Show ya Beyoncé Jijini Chicago
Tamasha la muziki lililojaa hamasa kubwa kutoka kwa malkia wa pop Beyoncé liligeuka kuwa eneo la sintofahamu baada ya mashabiki wake wawili kuingia katika ugomvi mkali karibu kabisa na jukwaa. Tukio hilo lilinaswa kwenye video na kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, likizua mijadala miongoni mwa mashabiki na wapenzi wa muziki. Katika video hiyo, ambayo sasa imevutia maelfu ya watazamaji, wanawake wawili wanaonekana wakitupiana maneno makali kabla ya kushikana mashati na kuanza kurushiana makonde yote hayo yakifanyika zikiwa ni mita chache kutoka mahali Beyoncé alikuwa akitumbuiza. Walinzi wa usalama walionekana wakijaribu kuingilia kati haraka, huku baadhi ya mashabiki wakisikitika kwa hali hiyo kuvuruga uzuri wa onyesho hilo. Mashabiki wengine waliokuwepo eneo hilo walisema mzozo huo huenda ulitokana na msongamano mkubwa karibu na jukwaa, ambapo kila mtu alikuwa akijaribu kupata nafasi nzuri ya kumwona Beyoncé kwa ukaribu zaidi. Watu wengi wamesikitishwa na tukio hilo, wakisema kuwa Beyoncé amekuwa mstari wa mbele katika kuhubiri upendo na umoja katika kazi zake za sanaa, hivyo haifai mashabiki wake kutenda kinyume na misingi hiyo. Hadi sasa, Beyoncé mwenyewe pamoja na timu yake ya usimamizi hawajatoa tamko rasmi kuhusiana na tukio hilo. Hata hivyo, vyombo vya usalama vya mji wa Chicago vimesema kuwa uchunguzi unaendelea na huenda hatua za kisheria zikachukuliwa kwa wahusika, hasa ikiwa walivunja sheria za usalama wa umma. Tamasha hilo lilikuwa sehemu ya ziara ya kimataifa ya Beyoncé ya CowBoy Carter na lilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki waliokuwa na matarajio makubwa ya kupata burudani ya kiwango cha juu ambayo licha ya tukio hilo dogo, bado ilifanyika kwa mafanikio makubwa.
Read More