Remy Ma Asisitiza Kumaliza Ndoa Kwa Heshima, Aahidi Kumlipa Wakili wa Papoose
Msanii mashuhuri wa muziki wa hip hop, Remy Ma, amevunja ukimya wake kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake na rapa mwenzake Papoose, akithibitisha kuwa bado mchakato wa talaka haujakamilika rasmi. Akizungumza kupitia matangazo ya moja kwa moja kwenye mtandao wa Instagram, Remy Ma alieleza kwa uwazi kuwa yuko tayari hata kugharamia ada za wakili wa Papoose ili kuhakikisha mchakato huo unakamilika kwa haraka na kwa utulivu. “Naweza hata kumlipia ada ya mwanasheria wake. Sitaki kuwa kikwazo katika maisha ya mtu,” alisema Remy kwa mtazamo wa amani na utu. Katika hatua nyingine, alijibu kauli za Claressa Shields, mpenzi wa sasa wa Papoose wakati wa mahojiano katika kipindi cha The Breakfast Club. Remy Ma alisema ingekuwa busara zaidi kwa Claressa kuomba mada hiyo kupuuzwa kwani ni ya faragha na bado iko kwenye mchakato wa kisheria. Alisisitiza kuwa hana chuki na hajawahi kuwa kikwazo kwa furaha ya Papoose. “Sijakasirika, wala sina chuki, lakini napenda kufafanua kuwa sina nia ya kumzuia Pap kupata furaha katika maisha yake. Sitaki simulizi za kupotosha ziendelee kusambazwa dhidi yangu,” alisisitiza. Kauli za Remy Ma zimepokelewa kwa mitazamo tofauti na wafuasi wake mitandaoni. Wengi wamepongeza namna alivyolishughulikia suala hilo kwa hekima na utu, huku wakisisitiza umuhimu wa watu kuachana kwa heshima bila kuzalishana visasi au migogoro isiyo ya lazima. Kwa sasa, mashabiki wa Remy Ma na Papoose wanasubiri kwa subira kuona hatima ya rasmi ya mchakato wa talaka hiyo, huku Remy akisisitiza kuwa lengo lake ni kuendeleza maisha kwa amani, bila kuathiri furaha ya mtu mwingine.
Read More