Koku Lwanga Atoa Ujumbe wa Hekima Kuhusu Ndoa na Uvumilivu
Mtengeneza maudhui kwenye mitandao ya kijamii, Koku Lwanga, amewasilisha ujumbe mzito wa hekima kuhusu ndoa na mahusiano, akisisitiza kuwa ndoa si rahisi kama inavyoonekana kwa nje, na hakuna anayejua jinsi ya kuimudu hadi awe ndani yake. Katika video ya awali ambayo imeibuka tena na kugonga vichwa vya habari mitandaoni, Koku anawahimiza watu kuwa na huruma, uvumilivu, na uelewa badala ya kuwahukumu wale wanaopitia changamoto au kuvunjika kwa ndoa zao. Koku amesema kuwa watu wengi huingia kwenye ndoa wakiwa na matumaini na malengo mema, lakini mara nyingi hukumbana na hali halisi ngumu ambayo haikuwa sehemu ya matarajio yao. Ametoa wito kwa jamii kuepuka lawama na kashfa, na badala yake kuonyesha msaada wa kihisia kwa wale wanaopitia nyakati ngumu. “Ndoa ni safari yenye milima na mabonde. Badala ya kuhukumu, tuwe na moyo wa kusaidia na kuelewa,” alisisitiza Koku. Ujumbe huu unakuja wakati ambapo ndoa ya Koku na mumewe Daddie Marto inaripotiwa kuwa kwenye mtikisiko, kufuatia madai ya usaliti. Koku anadaiwa kumshutumu Marto kwa kutoka nje ya ndoa yao, madai ambayo Marto ameyakanusha hadharani. Hali hiyo imeibua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii kuhusu maisha ya ndoa, huku wengi wakisifu msimamo wa Koku kwa kuchagua kutuma ujumbe wa hekima na si chuki, licha ya hali ngumu anayopitia.
Read More