Dyana Cods Aomba Radhi kwa Mashabiki Wake Kufuatia Kauli Zake Kuhusu Rais William Ruto
Msanii wa muziki wa rap nchini Kenya, Dyana Cods, ameomba msamaha hadharani kwa mashabiki wake kufuatia kauli zake za awali ambapo alionekana kuunga mkono Rais William Ruto. Taarifa hiyo ya msamaha iliitoa jukwaani kupitia video inayosambaa kwa kasi mitandaoni, ambapo Dyana alionekana akipiga magoti kwa hisia kubwa baada ya kumaliza kutumbuiza. Katika tukio hilo lililogusa hisia za wengi, Dyana alionesha majuto usoni mwake huku akiwatupia mashabiki wake maneno ya upendo na shukrani kwa kuwa upande wake licha ya makosa aliyoyafanya. Alisisitiza kuwa anawaweka mashabiki wake mbele kuliko kiongozi yeyote wa kisiasa, na kwamba anajali sana hisia zao. Msamaha huu unajiri baada ya hitmaker huyo wa ngoma ya “Set It” kushutumiwa mitandaoni kwa kauli zake za awali alizotoa akiwakosoa Wakenya kwa kumkosoa Rais Ruto kwa kushindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi. Kauli hiyo ilizua hisia kali, huku wengi wakimtuhumu kwa kujaribu kuhalalisha hali ngumu ya maisha nchini. Baadaye, Dyana alijitetea akisema alikuwa anatania. Tukio hili limeibua maoni tofauti mitandaoni, huku mashabiki wengine wakimsifu kwa ujasiri wa kukiri makosa yake, huku wengine wakimtaka awe makini zaidi na kauli zake hasa zinapohusisha masuala ya kisiasa yanayogusa hisia za wananchi wengi.
Read More