Gor Mahia Yapiga Kalamu Safu Yote ya Ufundi Kufuatia Msimu Mgumu
Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya FKF, Gor Mahia, wamefuta safu nzima ya ukufunzi, ikiwemo maafisa wa usalama wa timu, katika hatua ya kuimarisha benchi la kiufundi kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Kupitia taarifa rasmi, uongozi wa kilabu hicho umesema kuwa uamuzi huo umetokana na tathmini ya kina kuhusu utendaji wa timu msimu uliopita, na ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha uwezo wa kiufundi na ushindani wa timu hiyo. Hatua hiyo inajiri wakati Gor Mahia ikijaribu kujipanga upya baada ya msimu wa hali ya sintofahamu ulioandamana na mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, na matokeo ambayo hayakuwaridhisha mashabiki wake. Msimu uliopita, klabu hiyo ilipitia changamoto kubwa, ikiwemo kuajiri makocha watatu tofauti. Msimu ulianza chini ya kocha raia wa Kroatia, Sinisa Mihajlovic, ambaye aliteuliwa kuchukua nafasi ya Mbrasil Leo Neiva. Hata hivyo, Mihajlovic alitimuliwa baada ya kuhudumu kwa wiki chache pekee. Hatimaye, Zedekiah “Zico” Otieno aliingia na kushirikiana na kocha msaidizi Michael Nam, na kufanikisha Gor Mahia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi. Kwa sasa, mashabiki wa K’Ogalo wanatarajia kuona hatua madhubuti za kuirejesha timu hiyo kileleni mwa soka la Kenya msimu ujao.
Read More