Meja Kunta Atoa Msamaha kwa Jux na D Voice Baada ya Utata wa Wimbo
Baada ya drama ya muda mitandaoni kuhusu umiliki wa wimbo “Ex Wa Nani”, msanii wa singeli Meja Kunta amevunja ukimya na kutoa maoni yake juu ya sakata hilo, ambalo limewahusisha wasanii Jux na D Voice. Akizungumza na Podcast ya Simulizi na Sauti, Meja Kunta alieleza kuwa hana muda wa kubishana na watu anaowaita “watoto wadogo,” akionyesha msimamo wake wa kutotaka kuendeleza mzozo huo. “Mimi ni mkubwa, sikutaka kubishana na watoto wadogo. Sitaki kupigizana kelele. D Voice anajua mwenyewe alichokifanya na tumeshaongea jana,” alisema Meja Kunta kwa utulivu. Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Jux kuposti kipande cha wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii, hatua iliyozua maswali kutoka kwa mashabiki kuhusu uhalali wa wimbo huo, ambao awali ulitajwa kuwa ni mali ya Meja Kunta. Taarifa zinaeleza kuwa D Voice alimpa Jux wimbo huo bila ridhaa ya Meja, hali iliyochochea mvutano wa maneno. Hata hivyo, Meja Kunta ameonesha ukomavu kwa kufichua kuwa Jux na D Voice walimpigia simu kumuomba msamaha, jambo ambalo linaashiria kutamatika kwa mgogoro huo. Kwa sasa, mashabiki wanasubiri kuona hatma ya wimbo huo na iwapo utafanyiwa marekebisho ya umiliki au utaachiwa rasmi na mmoja wa wahusika waliotajwa.
Read More