Kanda Bongo Man Aomboleza Kifo cha Raila Odinga, Akumbuka Ukaribu Wake na Kenya
Msanii mkongwe wa muziki wa soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kanda Bongo Man, ameungana na Wakenya kuomboleza kifo cha aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Amolo Odinga. Kupitia ujumbe wake wa pole, Kanda Bongo Man ameonyesha huzuni kubwa kufuatia kifo cha kiongozi huyo ambaye amesema alikuwa mtu wa karibu kwake na mwenye upendo mkubwa kwa wasanii kutoka mataifa jirani. Msanii huyo amefichua kuwa Raila alikuwa kiongozi wa kwanza kumpokea jijini Nairobi alipowasili kwa mara ya kwanza nchini Kenya, kipindi ambacho Odinga alikuwa akihudumu kama Waziri Mkuu. Aidha, ameeleza kuwa Raila alimkaribisha mjini Kisumu, ambako alikuwa ameenda kutumbuiza kwenye hafla maalum ya kusherekea ushindi wa Barack Obama kama Rais wa Marekani mwaka 2008. Kanda Bongo Man, amesema kiongozi huyo alimfanya kuwa mgeni wake kwa siku kadhaa na kumpa malazi katika moja ya hoteli zake binafsi. Amesema atamkumbuka Raila kama kiongozi mwenye utu, mwenye mapenzi ya kweli kwa sanaa na watu wote bila kujali mipaka. Kwa miaka mingi, Kanda Bongo Man amekuwa na uhusiano wa kipekee na Kenya, taifa ambalo linachukuliwa kama nyumba yake ya pili. Muziki wake wa soukous na sebene umekuwa ukipendwa sana na mashabiki wa Kenya tangu miaka ya 1980, ambapo alitumbuiza katika matamasha makubwa jijini Nairobi, Mombasa, na Kisumu.
Read More