KayCyy Atikisa Mtandao kwa Ujumbe wa Kutafuta Mke

KayCyy Atikisa Mtandao kwa Ujumbe wa Kutafuta Mke

Msanii wa muziki wa hip hop mwenye asili ya Kenya, KayCyy, ameibua hisia na mjadala mitandaoni baada ya kutangaza kuwa anatafuta mke. Kupitia ujumbe wa moja kwa moja uliojaa hisia kwenye Insta stories yake, KayCyy alisema kuwa yuko tayari kwa mahusiano ya kudumu na anahitaji mtu wa kushirikiana naye katika safari ya maisha.  “Nahitaji mke Mungu. Kuna mengi juu yangu, nahitaji mtu wa kunisaidia kushinda dunia hii,”aliandika kwenye chapisho lake lililovutia mashabiki wengi. Ujumbe huo ulionyesha upande wake wa kibinadamu na hitaji la kuwa na mwenza wa maisha licha ya mafanikio yake ya kimuziki. KayCyy, ambaye jina lake halisi ni Mark Makora Mbogo, amejizolea umaarufu mkubwa Marekani na duniani kwa kushirikiana na majina makubwa kwenye tasnia ya muziki kama Kanye West, Lil Baby, Lil Wayne, Travis Scott na wengine wengi. Amehusika katika kutunga na kutekeleza miradi ya muziki yenye ushawishi mkubwa, ikiwemo albamu ya Donda ya Kanye West, ambayo ilimpa msanii huyo umaarufu zaidi. Licha ya mafanikio hayo ya kipekee, KayCyy sasa anaonesha kuwa mafanikio ya kweli kwake hayatakamilika bila upendo na mshirika wa maisha. Mashabiki wake kutoka Kenya na duniani wamejitokeza kwa wingi kuonyesha uungwaji mkono, huku baadhi wakijitolea kuwa “mke mtarajiwa” kupitia maoni ya mtandaoni. KayCyy ni miongoni mwa wasanii wachache wa asili ya Kenya waliopenya kwenye soko la muziki wa Marekani kwa mafanikio makubwa. Kutafuta mke kunaweza kuwa hatua mpya ya maisha ya kibinafsi kwa msanii ambaye tayari ameshavunja mipaka ya kimataifa kwenye muziki. Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama msanii huyo atapata mpenzi wa kweli atakayemsaidia “kushinda dunia” kama alivyoomba kwa Mungu.

Read More