Kenya Yaanza Vyema Mashindano ya Dunia ya Wavu wa Ufukweni Nchini Morocco

Kenya Yaanza Vyema Mashindano ya Dunia ya Wavu wa Ufukweni Nchini Morocco

Timu ya taifa ya mpira wa wavu wa ufukweni ya wanaume imeanza kwa kishindo kampeni yake kwenye Mashindano ya Dunia ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni yanayoendelea mjini Martiak, Morocco. Wachezaji wa Kenya, Brian Melly na Wilson Waibei, walionesha ubabe wao walipoibuka na ushindi wa seti mbili bila jibu dhidi ya wapinzani wao kutoka Burundi, Ishimwe na Ndayisaba, kwa alama 21-14 na 21-15 katika mechi ya kundi A. Hata hivyo, timu hiyo pia ilitoka sare na wenyeji Morocco katika mechi ya pili ya kundi hilo. Wachezaji wengine wa timu ya wanaume kutoka Kenya, Elphas Makuto na Jairus Kipkosgei, nao walitoa ushindani mkubwa kwa kutoka sare dhidi ya Ghana na Nigeria kwenye mechi zao za awali. Kwa upande wa wanawake, Kenya pia imetuma wakilishi wake kwenye mashindano hayo. Gaudencia Makokha na Sharlene Maywa wako katika kundi A pamoja na timu kutoka Nigeria na Burundi, ambapo wanatarajiwa kucheza mechi muhimu katika siku zijazo. Aidha, Mercy Iminza na Veronica Adhiambo watashuka uwanjani usiku wa leo kwenye kundi D wakikabiliwa na changamoto kutoka kwa timu za Nigeria na Mauritius. Mashindano haya ya dunia ni ya kiwango cha juu na yanatarajiwa kufikia kilele mwezi Novemba mwaka huu nchini Australia, ambako timu zitakazofanya vizuri zitajipatia nafasi ya kushiriki kwenye fainali hizo. Timu ya Kenya inaendelea kuonyesha dhamira ya kutwaa ushindi na kupeperusha vyema bendera ya taifa katika mchezo huu unaozidi kupata umaarufu barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Read More
 Kenya Kuandaa Fainali za CHAN 2025 Kasarani

Kenya Kuandaa Fainali za CHAN 2025 Kasarani

Kenya imepata nafasi ya kuwa mwenyeji wa fainali ya makala ya nane ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN), itakayochezwa tarehe 30 Agosti 2025 katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani. Hii ni mara ya kwanza kwa Kenya kuwa mwenyeji wa fainali ya mashindano haya ya kipekee barani Afrika. Mashindano hayo yataandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kenya, Tanzania na Uganda. Mechi ya ufunguzi itachezwa Dar es Salaam tarehe 2 Agosti, mechi ya nafasi ya tatu Kampala, na fainali kufanyika jijini Nairobi. Kenya itaongoza Kundi A litakalojumuisha Morocco, Angola, DR Congo na Zambia. Uwanja wa Kasarani unafanyiwa ukarabati mkubwa ili kufanikisha maandalizi ya fainali hiyo, ikiwemo maboresho ya taa, mfumo wa VAR, na huduma za mashabiki. Serikali kwa kushirikiana na FKF imeahidi kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa viwango vya kimataifa. Mashindano ya CHAN yanatoa jukwaa la kuibua vipaji vya wachezaji wa ndani, huku pia yakitarajiwa kuongeza mapato kupitia utalii na biashara. CAF inatarajiwa kutangaza ratiba kamili ya mechi na taratibu za tiketi hivi karibuni.

Read More
 KRG The Don Atoa Wito wa Amani Kati ya Kenya na Tanzania Kufuatia Kuzuia kwa Wanaharakati

KRG The Don Atoa Wito wa Amani Kati ya Kenya na Tanzania Kufuatia Kuzuia kwa Wanaharakati

Msanii na mfanyabiashara maarufu wa Kenya, KRG The Don, ametoa maoni yake kuhusu tukio la wanaharakati wa Kenya waliokamatwa na kuzuiliwa nchini Tanzania hivi karibuni. Akiwa na mtazamo wa kipekee, KRG amesema licha ya wanaharakati hao kudai kuwa walikuwa wakitetea haki, huenda hawakuzingatia mbinu sahihi za kuwasilisha ujumbe wao, jambo ambalo lilichangia wao kujipata matatani. “Ni kweli wanaharakati wana jukumu la kutetea haki, lakini kuna njia sahihi za kufanya hivyo. Kuna uwezekano walihusishwa na ajenda ya kumtetea kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Mbowe, na pengine walilipwa ili kusukuma ajenda hiyo,” alisema KRG. Aidha, KRG alieleza kusikitishwa na mzozo unaoendelea mitandaoni kati ya Wakenya na Watanzania kuhusu suala hilo. Amesisitiza kuwa Kenya na Tanzania ni mataifa ya kindugu, na haipaswi kuwa na mivutano ya kijamii au kisiasa. “Mimi nimekuwa nikisafiri Tanzania mara nyingi, na kila wakati nimepokelewa kwa heshima na mapenzi makubwa. Sioni sababu ya sisi kuchochea chuki kupitia mitandao ya kijamii,” aliongeza. Katika hatua nyingine, KRG amedokeza kuwa anapanga kusafiri hivi karibuni kwenda Tanzania kwa lengo la kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kutafuta muhula mwingine wa uongozi. Kauli ya KRG imepokewa kwa mitazamo tofauti mitandaoni, huku baadhi wakimpongeza kwa msimamo wake wa kuhimiza mshikamano wa Afrika Mashariki, na wengine wakitaka uchunguzi huru kuhusu hali ya wanaharakati waliokamatwa.

Read More
 Kenya Simbas Kwenda Afrika Kusini kwa Maandalizi ya Kombe la Dunia 2027

Kenya Simbas Kwenda Afrika Kusini kwa Maandalizi ya Kombe la Dunia 2027

Kikosi cha wachezaji 33 wa timu ya taifa ya Kenya ya rugby kwa wachezaji 15 kila upande, Kenya Simbas, kitasafiri kuelekea Afrika Kusini wiki hii kwa mazoezi ya kujiandaa na michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2027, itakayofanyika nchini Uganda. Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji wa uzoefu akiwemo nahodha George Nyambua, pamoja na Samuel Ovwamu, Collins Indeche, na waliorejea kikosini , John Okoth, Samuel Asati na Bethwel Anami,  waliokuwa sehemu ya kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2023 nchini Ufaransa. Kocha Jerome Paarwater amesema timu hiyo itachuana na vikosi mahiri kama SWD Eagles, Blue Bulls na Sanlam Boland Cavaliers. Simbas pia itajumuika na wakenya wanaocheza Afrika Kusini, David Bunduki na Thomas Okeyo, huku Hillary Mwanjilwa akitarajiwa kurejea baada ya kupona jeraha la muda mrefu.

Read More
 Msanii Chipukizi wa Kenya Njerae Afunguka Kuhusu Jinsi Alivyowahi Kuchukizwa na Jina Lake

Msanii Chipukizi wa Kenya Njerae Afunguka Kuhusu Jinsi Alivyowahi Kuchukizwa na Jina Lake

Msanii chipukizi mwenye kipaji kikubwa nchini Kenya, Njerae, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu hisia zake za awali dhidi ya jina lake la kisanii. Kupitia mahojiano ya hivi karibuni, Njerae alikiri kuwa aliwahi kuchukizwa na jina hilo, akisema hakulihusisha na ubunifu wala utambulisho aliotamani kuwa nao. “Nilikuwa nikipatwa na hasira kila nilipoitwa Njerae. Sikuwa nalipenda kabisa,” alieleza msanii huyo kwa uaminifu, akieleza kuwa wakati huo alitamani jina ambalo lingeonekana la kisasa zaidi au lenye mvuto wa kimataifa. Hata hivyo, muda ulivyopita na alivyoendelea kukua katika muziki wake, alianza kuona uzuri wa jina hilo na kulikubali kama sehemu ya utambulisho wake wa kipekee. Kulingana na Njerae, jina hilo sasa limempa nafasi ya kusimama tofauti katika tasnia ya muziki na limejengeka kama chapa yake binafsi. “Sasa hivi najivunia jina Njerae. Limekua sehemu yangu, na linawakilisha safari yangu, kutoka kwa mashaka hadi kujikubali na kujipenda,” alisema kwa msisitizo. Mashabiki wake wamepokea taarifa hiyo kwa moyo wa upendo na kumpongeza kwa uwazi wake, wakisema anaendelea kuwa mfano bora wa wasanii wanaojifunza kupenda asili na utambulisho wao. Njerae kwa sasa anaendelea kufanya vizuri katika muziki, na amekuwa akijizolea mashabiki wengi kutokana na mtindo wake wa kipekee na sauti ya kuvutia.

Read More
 Mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu ya Mpira wa Mikono Zazidi Kupamba Moto

Mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu ya Mpira wa Mikono Zazidi Kupamba Moto

Mechi za kuwania ubingwa wa ligi kuu ya mpira wa mikono nchini zinatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwenye uwanja wa Nyayo, huku kivumbi kikitarajiwa kati ya vinara wa ligi ya wanaume NCPB na wapinzani wao wakuu Equity. Timu zote mbili hazijapoteza mechi yoyote msimu huu, na mchezo wao unatarajiwa kuwa wa kuamua bingwa, hasa ikizingatiwa kuwa NCPB wana alama 46 huku Equity wakifuatia kwa alama 44 na mchezo mmoja mkononi. Katika mechi nyingine za wanaume, Ulinzi, waliopo nafasi ya tatu, watavaana na GSU, huku Strathmore wakikabiliana na Wakanda, wakilenga kumaliza msimu ndani ya tano bora. Ushindani mkali unatarajiwa, hasa kwa timu zinazotafuta nafasi ya kujihakikishia nafasi nzuri msimu ujao. Kwa upande wa ligi ya wanawake, Ulinzi Sharks watakutana na Daystar siku ya Jumapili, huku Young Zealots wakimenyana na NYS, na JKUAT wakichuana na Fireworks. Hadi sasa, Nairobi Water wanaongoza ligi hiyo kwa alama 26, wakifuatwa na Ulinzi Sharks na Daystar katika nafasi ya pili na tatu mtawalia.

Read More
 Daddy Owen Atoa Ushauri kwa Wanaume: “Usioe kwa Sababu ya Mapenzi, Oa kwa Sababu ya Kusudi”

Daddy Owen Atoa Ushauri kwa Wanaume: “Usioe kwa Sababu ya Mapenzi, Oa kwa Sababu ya Kusudi”

Msanii wa Injili nchini Kenya, Daddy Owen, ameibua mjadala mkubwa mtandaoni baada ya kutoa ushauri kwa wanaume kuhusu ndoa, akisisitiza kuwa msingi wa ndoa haupaswi kuwa mapenzi pekee, bali kuelewa kusudi la maisha. Kupitia chapisho lake la Instagram, msanii huyo alisema: “Kama mwanaume, usioe kwa sababu ya mapenzi. Oa kwa sababu ya kusudi. Nilifikiri ndoa ni kuhusu mapenzi, kumbe sio.” Msanii huyo alifafanua kauli yake kwa kusema kuwa wanaume wengi huingia kwenye ndoa wakiwa hawajajitambua wala kuelewa malengo yao ya maisha, hali inayochangia migogoro na kuvunjika kwa ndoa. “Kama kusudi lako halijajulikana, hiyo ni kama mabomu yanayosubiri kulipuka. Wanaume huoa chini ya kiwango chao kwa sababu hawajajua walipoelekea. Ukijua kusudi lako, mwanamke atajivuta kwenye hilo kusudi,” aliongeza. Kauli hii imepokewa kwa hisia tofauti kutoka kwa mashabiki wake, baadhi wakimsifu kwa mtazamo wa kiroho na msingi wa maisha yenye maono, huku wengine wakitofautiana naye, wakisema mapenzi bado yana nafasi kubwa katika ndoa yenye mafanikio. Daddy Owen, ambaye amepitia changamoto katika maisha yake ya ndoa hapo awali, anaonekana kutumia uzoefu wake kuwashauri vijana wanaopanga kuoa, akisisitiza umuhimu wa kujitambua kabla ya kuingia katika hatua hiyo muhimu ya maisha. Ujumbe wake umeendelea kuvutia mijadala kuhusu maana ya ndoa katika kizazi cha sasa, na umuhimu wa kuwa na msingi imara wa maisha kabla ya kuchukua jukumu la kifamilia.

Read More
 Kwa Uchungu na Ujasiri, Habida Aeleza Tukio Baya Zaidi Maishani Mwake

Kwa Uchungu na Ujasiri, Habida Aeleza Tukio Baya Zaidi Maishani Mwake

Msanii na mwigizaji wa Kenya, Habida, amefunguka kwa uchungu kuhusu tukio la kusikitisha zaidi kuwahi kumkumba maishani, akieleza kwa ujasiri kuwa aliwahi kubakwa na kwamba haoni haja ya kuficha ukweli huo. Katika mahojiano ya kina yaliyogusa hisia za wengi kupitia podcast ya SPM Buzz, Habida alisema kuwa bado haelewi kwa nini alitendewa ukatili huo, akisisitiza kuwa hakufanya jambo lolote lililostahili adhabu ya aina hiyo.  “Sikufanya chochote kilichompa haki ya kunitendea vile. Nilinyanyaswa kingono. Nimewahi kubakwa. Sifichi, kwa sababu hiyo ni sehemu ya safari yangu,” alisema kwa sauti ya utulivu lakini yenye uzito mkubwa. Habida alieleza kuwa kwa muda mrefu alibeba uzito wa kimya, lakini amejifunza kuwa kunyamaza huongeza maumivu na kumzuia mtu kupona. Sasa anatumia sauti yake kuwahamasisha wanawake na wanaume waliopitia unyanyasaji wa aina hiyo, kuzungumza na kutafuta msaada. “Najua kuna watu wengi waliopitia haya kama mimi. Nataka wajue hawako peke yao. Hatupaswi kuaibika kwa majeraha yaliyotusababishiwa na wengine,” aliongeza. Kauli ya Habida imeibua mjadala mpana mitandaoni kuhusu ukatili wa kijinsia na jinsi jamii inavyoshughulikia waathirika wa matukio hayo. Wengi wamepongeza ujasiri wake na kumtia moyo kwa kuchukua hatua ya kuongea hadharani, wakiitaka jamii iwe na huruma zaidi na kujenga mazingira salama kwa waathirika kutoa ushuhuda wao. Habida, anayejulikana kwa sauti yake ya kipekee na mchango wake mkubwa katika muziki wa Kenya, anaendelea kutumia jina lake kushawishi mabadiliko ya kijamii na kuinua wale waliovunjwa moyo kimya kimya.

Read More
 Shabiki Aweka Historia Kwenye Tamasha la Bien New York kwa Pendekezo la Ndoa la Kushtukiza

Shabiki Aweka Historia Kwenye Tamasha la Bien New York kwa Pendekezo la Ndoa la Kushtukiza

Tamasha la Bien jijini New York liligeuka kuwa jukwaa la mapenzi na mshangao, pale ambapo shabiki mmoja aliwashangaza wote kwa kutoa pendekezo la ndoa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo uliojaa hadi pomoni. Bien, mwanamuziki mahiri kutoka Kenya na mwanachama wa kundi maarufu la Sauti Sol, alikuwa akitumbuiza kwa hisia moja ya nyimbo zake za mahaba, alipokatizwa kwa heshima na shabiki huyo aliyepanda jukwaani akiwa ameambatana na mchumba wake. Kwa msaada wa timu ya Bien, alipanda jukwaani na kutangaza upendo wake hadharani kwa kutoa pendekezo la ndoa mbele ya mashabiki wote. Mashabiki walilipuka kwa shangwe na vigelegele wakati mwanamke huyo alikubali pendekezo hilo huku machozi ya furaha yakitiririka. Bien, alionekana kuguswa na tukio hilo la kipekee. “Hii ndiyo maana ya muziki – kuunganisha watu, kuleta mapenzi na kumbukumbu zisizosahaulika. Hongera kwa wapenzi wetu wapya!” alisema Bien Pendekezo hilo limekuwa gumzo mitandaoni, likipokelewa kwa furaha na msisimko na mashabiki kutoka kila kona ya dunia. Wengi wameelezea tukio hilo kama moja ya matukio ya kipekee kuwahi kutokea katika tamasha la muziki, na ushahidi kuwa muziki wa Bien si tu wa kusikiliza bali pia wa kuishi. Tamasha hilo lilikuwa sehemu ya ziara ya kimataifa ya Bien kama msanii wa kujitegemea, na sasa linaacha kumbukumbu si tu kwa sababu ya muziki mzuri, bali pia kwa kuwa sehemu ya safari ya mapenzi ya watu wawili.

Read More
 Siasa si Majina, ni Maendeleo – Ujumbe wa Octopizzo kwa Wakenya

Siasa si Majina, ni Maendeleo – Ujumbe wa Octopizzo kwa Wakenya

Msanii maarufu wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Octopizzo, ameibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha ujumbe mzito katika mtandao wa X (zamani Twitter), akiwataka Wakenya wawe makini na hali ya kisiasa nchini. Kupitia ujumbe huo, Octopizzo amewataka raia kukataa kile alichokiita usahaulifu wa kisiasa, akieleza kuwa upinzani unaojitokeza hivi sasa si mpya kwa kweli, bali unaundwa na viongozi waliowahi kushika nyadhifa serikalini kwa muda mrefu bila kuleta maendeleo ya maana kwa taifa. “Wakenya hawapaswi kusahau historia ya kisiasa. Huu unaoitwa upinzani mpya ni mkusanyiko wa viongozi waliokataliwa, au waliodumu serikalini kwa zaidi ya miaka ishirini bila kuwa na mafanikio yoyote ya kushikika. Wanaonekana kutamani madaraka, si mageuzi ya kweli,” ameandika msanii huyo. Octopizzo ameendelea kwa kutoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kutanguliza maendeleo ya taifa badala ya kushabikia watu binafsi au vyama. “Tuwe waangalifu na tujitolee kwa maendeleo, si kwa kushabikia watu au majina. Kama taifa, tunastahili uongozi unaowajali wananchi si wakati wa uchaguzi pekee, bali kila siku.” Ameongeza kwa msisitizo. Ujumbe huu umepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni, baadhi ya wananchi wakimsifu kwa kutoa kauli yenye busara na ujasiri,huku wengine wakitumia fursa hiyo kujiuliza maswali kuhusu mwelekeo wa kisiasa nchini. Hii si mara ya kwanza kwa Octopizzo kutoa maoni kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa, kwani amekuwa akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kuhamasisha umma kuhusu haki, uwajibikaji, na maendeleo ya vijana nchini.

Read More
 Bien Aandika Historia The Radar Radio, Awasilisha Utambulisho wa Mkenya kwa Ubunifu

Bien Aandika Historia The Radar Radio, Awasilisha Utambulisho wa Mkenya kwa Ubunifu

Msanii maarufu kutoka Kenya na mmoja wa wanamuziki wa kundi la Sauti Sol, Bien-Aimé Baraza, ameweka historia mpya kwa kuwakilisha Kenya na Afrika Mashariki kwenye kipindi maarufu cha The Radar Radio nchini Uingereza. Hii ni baada ya kuonekana kwenye kipindi hicho kwa freestyle ya kipekee, akifuatia nyayo za msanii Kaycyy, ambaye alikuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushiriki. Kilichoifanya freestyle ya Bien kuwa ya kipekee si tu uwezo wake wa kutunga na kuwasilisha kwa ustadi, bali pia hatua yake ya kuleta kuku hai studio kama ishara ya utamaduni wake wa Kiluhya na mzizi wake wa Kiafrika. Hatua hiyo imetafsiriwa kama tamko la fahari ya utambulisho wake wa asili, na imepokelewa kwa hisia tofauti mitandaoni. The Radar Radio ni jukwaa maarufu duniani ambalo limewahi kuwakaribisha wasanii wakubwa kama Drake, Central Cee, Ice Spice na wengine wengi, likiwa ni sehemu ya kuonesha vipaji halisi kupitia maonyesho ya freestyle. Kwa Bien, huu ulikuwa wakati wa kuonesha kuwa muziki wa Afrika Mashariki unaweza kusimama bega kwa bega na muziki wa kimataifa, huku ukidumisha mizizi ya kitamaduni. Hatua yake imepongezwa sana na mashabiki barani Afrika na diaspora, wengi wakisema kuwa ni mfano bora wa jinsi wasanii wa Kiafrika wanavyoweza kutumia jukwaa la kimataifa kueneza utamaduni wao kwa njia ya ubunifu. Bien kwa sasa anaendelea na kazi yake ya muziki kama msanii wa kujitegemea baada ya mafanikio makubwa akiwa na Sauti Sol. Uwepo wake kwenye The Radar ni hatua nyingine kubwa katika safari yake ya kimataifa.

Read More
 “Siku Moja Tutazungumza Kuhusu ‘Diddy’ wa Kenya” – Rapper Wangechi Afichua Mada Nzito Kuhusu Tasnia ya Muziki

“Siku Moja Tutazungumza Kuhusu ‘Diddy’ wa Kenya” – Rapper Wangechi Afichua Mada Nzito Kuhusu Tasnia ya Muziki

Msanii wa muziki wa rap nchini Kenya, Wangechi, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kuandika ujumbe wa kutatanisha unaoashiria kuwepo kwa unyonyaji na hujuma dhidi ya wasanii wa kike katika tasnia ya muziki humu nchini. Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Wangechi alidokeza kuwa kuna mtu mashuhuri kwenye sekta ya muziki humu nchini anayefanana na mtayarishaji wa muziki wa Marekani, Diddy ambaye kwa miaka amezuia wasanii wa kike kutoka na kazi zao kutoka studio. “One day we shall speak about the Diddy of Kenya and how no female artist ever left that studio with their music.” (“Siku moja tutazungumza kuhusu Diddy wa Kenya na jinsi hakuna msanii wa kike aliyewahi kutoka katika studio hiyo na muziki wake.”) – aliandika Wangechi. Ingawa hakumtaja mtu yeyote kwa jina, kauli hiyo imeibua mijadala mikubwa kuhusu usalama, haki na usawa katika sekta ya muziki hasa kwa wasanii wa kike ambao kwa muda mrefu wamelalamikia ukosefu wa usaidizi wa haki na kuwepo kwa mazingira yenye unyanyasaji wa kiakili, kijinsia na kitaaluma. Mashabiki na wadau wa muziki wameanza kujiuliza ni nani “Diddy wa Kenya” anayetajwa, huku wengi wakihusisha ujumbe huo na visa vya awali vilivyoripotiwa na baadhi ya wanamuziki wachanga. Hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, Wangechi bado hajatoa maelezo zaidi, lakini ujumbe wake umeacha gumzo zito ambalo huenda likabadilisha mwelekeo wa mazungumzo kuhusu usalama, uhuru na haki za wasanii wa kike nchini Kenya.

Read More