Kenya Simbas Kwenda Afrika Kusini kwa Maandalizi ya Kombe la Dunia 2027
Kikosi cha wachezaji 33 wa timu ya taifa ya Kenya ya rugby kwa wachezaji 15 kila upande, Kenya Simbas, kitasafiri kuelekea Afrika Kusini wiki hii kwa mazoezi ya kujiandaa na michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2027, itakayofanyika nchini Uganda. Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji wa uzoefu akiwemo nahodha George Nyambua, pamoja na Samuel Ovwamu, Collins Indeche, na waliorejea kikosini , John Okoth, Samuel Asati na Bethwel Anami, waliokuwa sehemu ya kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2023 nchini Ufaransa. Kocha Jerome Paarwater amesema timu hiyo itachuana na vikosi mahiri kama SWD Eagles, Blue Bulls na Sanlam Boland Cavaliers. Simbas pia itajumuika na wakenya wanaocheza Afrika Kusini, David Bunduki na Thomas Okeyo, huku Hillary Mwanjilwa akitarajiwa kurejea baada ya kupona jeraha la muda mrefu.
Read More