Bahati Awashukuru Mashabiki kwa Kumpongeza kwa Muonekano Mpya Licha ya Video Kuzua Maswali
Mwanamuziki wa Kenya, Bahati, amezua gumzo mitandaoni baada ya kuwashukuru mashabiki wake kwa pongezi walizompa kuhusu muonekano wake mpya bila nywele. Kupitia video aliyochapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Bahati alidai kuwa alinyoa rasta zake kufuatia kichapo cha timu yake ya Arsenal mikononi mwa PSG, katika mechi ya hivi karibuni ya UEFA Champions League. Katika ujumbe wake kwa mashabiki, Bahati alisema: “Nimeanza kujipenda zaidi bila nywele. Nimejifunza kuwa upendo wa kweli huanza na wewe mwenyewe.” Hata hivyo, kilichozua utata ni ubora wa video hiyo, ambayo inaonyesha mabadiliko ya haraka ya uhariri (transition), huku dreadlocks zake zikiendelea kuonekana kwa vipindi tofauti ndani ya video hiyo. Baadhi ya mashabiki walihoji iwapo alinyoa kweli au kama ilikuwa ni kiki ya mitandao. Katika sehemu ya maoni, baadhi ya mashabiki walitoa pongezi wakisema muonekano wake mpya unampendeza na unampa sura ya “umakini mpya”, huku wengine wakitilia shaka ukweli wa madai yake. “Bahati hata kama ni kiki, umetuburudisha. Ila tuambie ukweli – hizo rasta bado zipo ama?” aliandika mmoja wa mashabiki. Muimbaji huyo, anayejulikana kwa kubadili mitindo ya maisha hadharani, ameendelea kuvutia vichwa vya habari kwa sababu mbalimbali kuanzia maisha ya ndoa, siasa, hadi mitindo ya uvaaji. Sasa, inaonekana hata nywele zimeingia kwenye orodha ya vitu vinavyoleta mjadala. Hadi sasa, Bahati hajatoa kauli rasmi kuhusu video hiyo au kama kweli alinyoa, lakini haijazuia mashabiki wake kuendelea kutoa maoni mseto kati ya wanaomsifu na wanaohoji ukweli wa mabadiliko yake
Read More