Kings Music Watoa Tamko Kuhusu Kuondolewa kwa Video ya King Kiba
Uongozi wa Kings Music Records wametoa tamko rasmi kuhusu tukio la kuondolewa kwa video ya wimbo maarufu wa King Kiba, Ubuyu, kutoka kwenye mtandao wa YouTube masaa machache tu baada ya kupandishwa tarehe 3 Julai, Alhamisi iliyopita. Kwa mujibu wa tamko hilo, uondoaji wa video hiyo ulitokana na vitendo vya watu wasioidhinishwa waliotumia mfumo wa kuripoti ukiukaji wa hakimiliki kwa makusudi vibaya, wakitumia majina ya uongo na madai yasiyo halali. “Tunatilia mkazo kuwa madai haya ya mtu wa tatu dhidi ya kazi yetu ni ya uongo, ya kuhuzunisha na hayakubaliki kabisa,” limesema andiko la Kings Music Records. Tukio hili limeleta taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki wa Bongo Flava, huku Kings Music Records wakisisitiza kwamba madhara yaliyosababishwa kwa msanii na biashara yao ni makubwa sana. “Hili si tu usumbufu wa kitaalamu, bali pia ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya uadilifu wa kisanaa, uaminifu wa hadhira, na maisha ya wasanii katika sekta ya ubunifu,” limesisitizwa. Aidha, Kings Music Records wamesema tayari wameanzisha uchunguzi wa kisheria dhidi ya tukio hili na kwamba yeyote atakayebainika kushiriki katika udanganyifu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria. “Hali hii si tishio kwa Alikiba peke yake, bali ni tishio kwa mfumo mzima wa ubunifu,” limesema tamko hilo. Ingawa ushindani ni sehemu ya kawaida katika tasnia ya muziki, kampuni hiyo imelaani vikali vitendo vya hila na udanganyifu kama hivi, kwa niaba ya wasanii na wabunifu wa muziki, hasa kwa lengo la kulinda hadhi ya Bongo Flava na tasnia ya muziki nchini Tanzania. Kwa mashabiki wa King Kiba, Kings Music Records wamesisitiza wanawashukuru kwa subira yao, sapoti thabiti, na imani katika nguvu ya muziki. Pia wametoa shukrani za dhati kwa wote waliochangia kutatua suala hili kwa haraka, haki na ushirikiano.
Read More