Linex Mjeda Avamiwa Nyumbani, Apoteza Mali na Fedha Milioni 6

Linex Mjeda Avamiwa Nyumbani, Apoteza Mali na Fedha Milioni 6

Mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva na muziki wa Injili, Linex Sunday Mjeda, amepatwa na tukio la kusikitisha baada ya kuvamiwa na kuporwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia leo katika eneo la Sala Sala, jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa rasmi aliyoitoa kupitia mitandao ya kijamii, watu wasiojulikana walivamia makazi yake na kuiba mali mbalimbali zikiwemo runinga (TV), mfumo wa muziki wa nyumbani (music system), vifaa vya studio ya kurekodia nyumbani pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 6. “Nimepoteza kila kitu muhimu nilichokuwa nimejenga kwa juhudi zangu zote. Studio yangu, vifaa vya muziki, na fedha taslimu zimechukuliwa usiku wa kuamkia leo. Ni wakati mgumu sana kwangu,” aliandika Linex kwa masikitiko. Mwanamuziki huyo, ambaye kwa miaka ya hivi karibuni ameonesha mwelekeo mkubwa kwenye muziki wa Injili na kusaidia vijana chipukizi kupitia studio yake, amesema tukio hilo limeacha athari kubwa si tu kwake binafsi, bali pia kwa kazi zake za kila siku. Kutokana na tukio hilo, Linex ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika maeneo ya Sala Sala na maeneo mengine ya pembezoni mwa jiji ambayo yamekuwa yakikumbwa na matukio ya uhalifu. “Naomba Jeshi la Polisi lifuatilie suala hili kwa makini na kuhakikisha usalama unaimarishwa. Hali ya wizi mitaani inazidi kuwa tishio, hasa kwa sisi tunaofanya kazi za sanaa na kuwekeza majumbani,” aliongeza. Tukio hilo limeibua hisia mseto miongoni mwa mashabiki wake na wadau wa sanaa, ambao wameonesha masikitiko na kutoa pole kupitia mitandao ya kijamii, wakimtaka Linex aendelee kuwa imara licha ya tukio hilo la kusikitisha. Mpaka sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, lakini inatarajiwa kuanza uchunguzi mara moja ili kubaini waliohusika na kusaidia kurejesha mali zilizopotea.

Read More
 Linex Ahamasisha Wasanii Walioathirika Kisaikolojia Kuendelea na Muziki

Linex Ahamasisha Wasanii Walioathirika Kisaikolojia Kuendelea na Muziki

Msanii wa Bongo Fleva, Linex Sunday Mjeda, ametuma ujumbe kupitia InstaStory akiwashauri wasanii wanaokumbwa na changamoto za afya ya akili, hususan msongo wa mawazo, kurudi studio na kuendelea na kazi zao za sanaa. Katika ujumbe wake, Linex alionesha kusikitishwa na hali ya baadhi ya wasanii kupotea kwenye muziki kutokana na matatizo ya kiakili. Alisisitiza kuwa kazi ya sanaa ni tiba na njia muhimu ya kupambana na changamoto za maisha, akihimiza kuwa kazi haidanganyi. “Wanaopitia magonjwa ya akili kwenye muziki/sanaa, huwa mmefanyiwa makubwa yapi mpaka mpagawe na mshindwe kurudi studio? Em rudini studio, fanyeni kazi – kazi haisemagi uongo. Depression my mxiiiiiiiieww…,” alisema kupitia ujumbe wake uliojaa hisia Instagram. Kauli ya msanii huyo imeibua maoni mseto kutoka kwa mashabiki na wadau wa sanaa, wengine wakiona ni wito wa kuhamasisha, huku wengine wakihisi kuwa masuala ya afya ya akili yanahitaji kuangaliwa kwa makini na kwa huruma zaidi. Katika miaka ya karibuni, wasanii kadhaa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wamekuwa wakifunguka kuhusu changamoto za kiakili wanazopitia, huku mashabiki na wanaharakati wakizidi kutoa wito kwa jamii kuwa na uelewa zaidi kuhusu afya ya akili. Ujumbe wa Linex umetafsiriwa na wengi kama wito kwa wasanii kuendelea kupambana na kutafuta uponyaji kupitia kazi zao za muziki na sanaa.

Read More
 LINEX SUNDAY MJEDA AACHIA EP YAKE MPYA

LINEX SUNDAY MJEDA AACHIA EP YAKE MPYA

Msanii wa Bongofleva Linex Sunday Mjeda ameachia rasmi EP yake mpya ya nyimbo za Dini, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tofauti na alivyozoeleka akiimba nyimbo za kidunia. EP hiyo ambayo ameipa jina la My Side B ina jumla ya nyimbo 4 za moto ambazo amezifanya bila kumshirikisha msanii yeyote. EP hiyo ina nyimbo kama “Umepotea”, “Mtetezi”, “Utaniona” na “Tusafishe” na inapatikana ‘Exclusive’ kupitia mtandao wa kukisikiliza na kupakua muziki wa Boomplay. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Linex amesema kwamba alikuwa na ndoto ya kutoa kazi yenye nyimbo za dini, hivyo amefurahi kuona ametimiza ndoto yake hiyo. My side b ni EP ya tatu kwa mtu mzima Linex tangu aanze safari yake ya muziki  baada ya tatu za mjeda ep ya mwaka wa 2021 na dunia nyingine ya mwaka wa 2020.

Read More
 LINEX MBIONI KUACHIA EP YENYE NYIMBO ZA DINI

LINEX MBIONI KUACHIA EP YENYE NYIMBO ZA DINI

Nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Linex Mjeda yupo mbioni kuachia EP yake mpya ya nyimbo za Dini, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tofauti na alivyozoeleka akiimba nyimbo za kidunia. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Linex amezungumzia ujio wa EP yake, kwa kusema kwamba alikuwa na ndoto ya kutoa kazi yenye nyimbo za dini, hivyo amefurahi kuona ametimiza ndoto yake hiyo. EP ambayo ameipa jina la ‘MY SIDE B’  ina jumla ya ngoma 4, ambazo ni “Umepotea”, “Mtetezi”, “Utaniona” na “Tusafishe”. Katika upande wa Bongo Fleva msanii Linex hivi karibuni aliachia ngoma yake iitwayo “Sawa Baby” akiwa amemshirikisha Pallaso ambayo pia imefanikiwa kufanya vizuri katika mtandao wa Youtube.

Read More