Bien na Matata Wauza Tiketi Zote Paris, Waweka Historia Mpya ya Muziki wa Kenya
Wasanii nyota wa Kenya Bien-Aimé Baraza (maarufu kama Bien) na kundi la Matata wameweka historia kwa kuuza tiketi zote katika onyesho lao la muziki lililofanyika mjini Paris, Ufaransa, Ijumaa usiku hatua inayotajwa kama ushindi mkubwa kwa muziki wa Kenya kimataifa. Tamasha hilo lililoandaliwa katika ukumbi maarufu wa La Bellevilloise, ulioko katikati ya jiji la Paris, liliwaleta pamoja mamia ya mashabiki kutoka mataifa mbalimbali waliokuwa na hamu ya kushuhudia utambulisho wa muziki wa Kenya kuanzia Afro-pop ya Bien hadi dansi na miondoko ya Matata. Bien, ambaye ni mwanachama wa zamani wa kundi la Sauti Sol, alitumbuiza kwa nyimbo maarufu kama Inauma, Dimension na Too Easy, huku kundi la Matata likiwasha jukwaa kwa mitindo yao ya kipekee inayochanganya Gengetone, Afrobeat na Hip-hop ya kisasa. Kwa mujibu wa waratibu wa tamasha hilo, tiketi zote ziliisha siku chache kabla ya onyesho hilo, ishara ya kupanda kwa umaarufu wa muziki wa Kenya katika soko la kimataifa. Wakenya wanaoishi ughaibuni walijitokeza kwa wingi, wengi wao wakijivunia kuona wasanii kutoka nyumbani wakipeperusha bendera ya Kenya kwa ufanisi mkubwa. Mitandao ya kijamii ilifurika na video za mashabiki wakicheza kwa furaha, huku wakisifia ubora wa muziki na utumbuizaji wa hali ya juu. Matukio kama haya yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kutangaza muziki wa Afrika Mashariki duniani, hasa wakati ambapo wasanii wa Nigeria na Afrika Kusini wamekuwa wakitawala majukwaa ya kimataifa.
Read More