MCSK Yaonya Kumbi za Burudani Zinazopuuza Wasanii Walio na Leseni
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK), Dkt. Ezekiel Mutua, ametoa onyo kali kwa wamiliki wa kumbi za burudani, hoteli na maeneo ya umma yanayopiga muziki, akiwataka kutoepuka au kuwatenga wasanii walio na leseni halali. Kupitia taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari, Dkt. Mutua alisema kuwa baadhi ya maeneo ya burudani yamekuwa yakikiuka haki za wasanii kwa kupiga nyimbo zao bila kufuata taratibu za leseni, au kwa kuandaa matukio bila kushirikisha wanamuziki waliojisajili kisheria. “Maeneo yanayoendelea kuwasiliti wasanii na kutumia kazi zao bila leseni yako katika hatari ya kupokonywa kibali cha kupiga muziki wenye hakimiliki,” alionya Mutua. Amesisitiza kuwa MCSK itaongeza ukaguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote wanaokiuka sheria za hakimiliki, ili kuhakikisha kuwa wasanii wanalindwa na kunufaika na kazi zao. Onyo hili linajiri wakati ambapo mjadala kuhusu malipo duni kwa wasanii unazidi kushika kasi, huku wasanii wengi wakilalamika kwamba kazi zao zinatumika kibiashara bila wao kufaidika ipasavyo. Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya kimehimiza waandaaji wa matukio, DJ’s, na wamiliki wa biashara kuhakikisha kuwa wanashirikiana na wasanii walio na leseni na kulipia matumizi ya muziki ili kuunga mkono ukuaji wa tasnia ya muziki nchini.
Read More