Sammy Boy Akanusha Taarifa za Gari Lake Aina ya Mercedes Benz GLE 53 Kupigwa Mnada

Sammy Boy Akanusha Taarifa za Gari Lake Aina ya Mercedes Benz GLE 53 Kupigwa Mnada

Msanii na Mjasiriamali kutoka nchini Kenya, Sammy Boy, amezungumza wazi kuhusu uvumi ulioenea kwamba gari lake la kifahari aina ya Mercedes Benz GLE 53 lilipigwa mnada kwa sababu ya matatizo ya kifedha. Katika video aliyoshiriki kwenye ukurasa wake wa Instagram, Sammy Boy amekanusha vikali madai hayo, akieleza kuwa gari hilo halikupigwa mnada bali alilirejesha kwa muuzaji mwenyewe baada ya kugundua kuwa lilikuwa na matatizo ya gearbox (gia) yaliyokuwa yakijirudia mara kwa mara. “Nilinunua gari hilo kwa uaminifu mkubwa, lakini baada ya muda mfupi nilianza kupata changamoto kwenye mfumo wa gia. Baada ya mashauriano na muuzaji, niliamua kulirudisha kwa hiari ili kuepuka matatizo zaidi,” alieleza Sammy Boy. Sammy By ambaye pia ni Mshawishi maarufu wa mitandao ya kijamii, amesisitiza kuwa hatua hiyo haikuwa kwa sababu ya matatizo ya kifedha kama inavyodaiwa mitandaoni, bali ni uamuzi wa kibiashara na wa kiusalama. Aliongeza kuwa bado anaendelea na shughuli zake za biashara kama kawaida na hana deni lolote linalohusiana na gari hilo. Mashabiki wake wengi wameonyesha kumuelewa na kumpongeza kwa uwazi wake, huku wengine wakihimiza umuhimu wa wanasoshalaiti kuwa wa kweli na kufafanua mambo yanapovuma mtandaoni. Hata hivyo kampuni iliyomuuza gari hilo haijatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo hadi sasa.

Read More