Morocco na Misri Karibu na Tiketi ya Kombe la Dunia
Morocco na Misri zina nafasi kubwa ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, kufuatia mwenendo wao mzuri katika mechi za kufuzu zinazoendelea barani Afrika. Mashindano haya ya kufuzu, yaliyoanza mwezi Novemba 2023, yanatarajiwa kukamilika mwezi ujao, huku raundi nne muhimu zikiwa zimebaki. Katika mfumo wa kufuzu wa Afrika, ni washindi wa makundi tisa pekee watakaopata nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Timu nyingine nne bora zitakazomaliza katika nafasi ya pili zitapata nafasi ya pili kupitia mchujo wa mabara unaotarajiwa kuchezwa Novemba mwaka huu. Misri na Morocco, ambazo zimekuwa na kampeni imara hadi sasa, huenda zikajikatia tiketi zao moja kwa moja kabla ya raundi ya mwisho, iwapo zitapata ushindi katika mechi zao za wiki hii. Ushindi huo utazifanya ziendelee kuongoza makundi yao kwa tofauti ya alama isiyoweza kufikiwa na wapinzani wao katika mechi zilizobaki. Timu nyingine kama Cape Verde, Comoro na Sudan bado zina nafasi ya kufuzu, japo zinahitaji ushindi katika mechi zao zilizosalia. Kwa upande mwingine, Nigeria, ambayo ni moja ya mataifa yaliyotarajiwa kufanya vizuri, inakumbwa na presha kubwa na huenda ikaondolewa mapema ikiwa haitarejea kwenye mstari wa ushindi.
Read More