Nameless Amwaga Sifa kwa Msanii Chipukizi kwa Kufanya Cover ya Nasinzia
Msanii mkongwe wa muziki kutoka Kenya, Nameless, amemwagia sifa msanii chipukizi Lafayette baada ya kuimba kwa ustadi cover ya wimbo wake uitwao Sinzia. Hii ni baada ya Cover hiyo kupokelewa vyema mtandaoni, huku mashabiki wakisifu ubunifu na uimbaji wa msanii huyo mpya kwenye tasnia. Kupitia Instastory kwenye mtandao wa Instagram, Nameless ameonyesha furaha yake kuona kizazi kipya cha wasanii kikichukua hatua kubwa katika muziki, akisema kuwa ni jambo la kutia moyo kuona vipaji vipya vikionyesha ubunifu na kuheshimu kazi za wasanii waliotangulia. Amehimiza Lafayette kuendelea na safari yake ya muziki akimtakia baraka katika njia yake. Wimbo Sinzia, uliotolewa mwaka 2006, ni moja ya ngoma zilizotikisa sana na kuacha alama katika mizani ya muziki wa Kenya. Kwa zaidi ya miaka 18, wimbo huo umeendelea kuwa kipenzi cha mashabiki na kuchezwa kwenye matamasha, redioni na majukwaa mbalimbali. Sifa za Nameless kwa Lafayette zinaonekana kuwa motisha kwa wasanii vijana wanaochipukia, wakithibitisha kuwa vipaji vipya vina nafasi kubwa katika kubadilisha na kukuza muziki wa Kenya.
Read More