Timaya: “Muziki Si Rahisi Tena, Wimbo Mmoja Unahitaji $100K
Mwimbaji nguli wa muziki wa Afrobeats kutoka Nigeria, Timaya, amefichua changamoto kubwa inayowakumba wasanii katika sekta ya muziki, hasa linapokuja suala la kukuza kazi zao. Akiwa kwenye mahojiano ya hivi karibuni, Timaya alisema enzi zimebadilika sana, na kwamba mafanikio katika muziki kwa sasa yanahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha. Amefichua kuwa kwa sasa, msanii anayelenga kufanikisha wimbo mmoja kimafanikio, anahitaji bajeti isiyopungua dola 100,000 za Marekani. “To promote just one song, you need nothing less than $100k. That’s the world we live in now,” alisema Timaya kwa msisitizo. Mwanamuziki huyo ambaye alitamba na nyimbo kama “I Can’t Kill Myself,” “Balance” na “Cold Outside” aliweka wazi kuwa mafanikio hayategemei tena kipaji pekee, bali pia uwezo wa kifedha, mikakati ya kibiashara na nguvu ya usambazaji kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kauli hiyo imezua mjadala mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakikubaliana naye kwa kusema muziki wa sasa ni kama biashara nyingine yoyote, inayohitaji mtaji, ilhali wengine wakisema gharama hizo kubwa zinaweka vizingiti kwa vipaji vipya vinavyochipukia. Hata hivyo, Timaya amesisitiza kuwa ingawa njia ya mafanikio si rahisi, wasanii wanapaswa kujifunza kuweka mikakati ya kibiashara sambamba na ubunifu wao ili kufanikisha ndoto zao katika tasnia ya muziki.
Read More