Njerae Aahirisha Lover Girl’s Tour ya Australia Kufuatia Changamoto za Visa
Msanii maarufu wa Afro-R&B kutoka Kenya, Njerae, ametangaza kuahirishwa kwa ziara yake ya Lover Girl’s Tour nchini Australia kufuatia changamoto zisizotarajiwa za mchakato wa visa. Kupitia taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye mitandao yake ya kijamii, Njerae alieleza kuwa kucheleweshwa kwa mchakato wa visa kumeathiri ratiba ya ziara hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wake nchini humo. “Ziara ya Lover Girl’s Tour huko Australia imeahirishwa kwa sababu ya ucheleweshaji wa visa, jambo ambalo liko nje ya uwezo wetu kwa sasa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo. Tangazo hilo limepokewa kwa masikitiko na wafuasi wa Njerae kutoka Australia waliokuwa tayari wamejikatia tiketi kuhudhuria tamasha hilo lililotarajiwa kuandaliwa kwenye miji kadhaa ikiwemo Sydney na Melbourne. “Tunajua wengi wenu mlikuwa mnasubiri kwa hamu, nasi tunahisi maumivu hayo pamoja nanyi. Tunafanya kazi kwa karibu kuhakikisha kuwa tarehe mpya zinapangwa,” Njerae aliongeza. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tiketi zote zilizotolewa zitaendelea kuwa halali kwa tarehe mpya zitakapotangazwa rasmi. Hata hivyo, kwa wale wanaopendelea kurejeshewa fedha zao, wanaombwa kujibu barua pepe waliopokea tiketi kupitia kwake ili mchakato huo ufanyike kwa haraka. Njerae alimalizia kwa kuwashukuru mashabiki kwa uelewa wao na kuahidi kuwa ziara hiyo itarudi kwa nguvu zaidi pindi taratibu za visa zitakapokamilika. “Asanteni kwa kuendelea kutupa moyo. Hatuwezi kusubiri kuwaona hivi karibuni,” alihitimisha.
Read More