Samidoh Aingia Matatani Baada ya Kushiriki Nderemo za ‘Wantam’ Klabuni

Samidoh Aingia Matatani Baada ya Kushiriki Nderemo za ‘Wantam’ Klabuni

Mwanamuziki na afisa wa polisi, Konstebo Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, anaripotiwa kuwa katika hatari ya kupoteza ajira yake baada ya kushiriki nderemo na vifijo vya “Wantam” akiwa kwenye klabu ya burudani. Kwa mujibu wa Huduma ya Polisi Nchini (NPS), Samidoh anadaiwa kukiuka mwongozo rasmi unaodhibiti mwenendo wa maafisa wa polisi, hata wanapokuwa nje ya majukumu ya moja kwa moja. NPS imethibitisha kuwa suala hilo linachunguzwa, na endapo Samidoh atapatikana na hatia, anaweza kuadhibiwa kwa njia mbalimbali, zikiwemo kupokonywa wadhifa, kuhamishwa kituo, kutozwa faini, kupewa onyo la kinidhamu au hata kuachishwa kazi kabisa. Tukio hilo limezua maoni mseto mitandaoni, huku mashabiki wake wakimiminika mitandaoni kumuunga mkono kwa kusema ana haki ya kuwa na maisha ya kibinafsi nje ya kazi. Wengine hata wameeleza kuwa Samidoh ni kiungo muhimu katika kuunganisha jamii kupitia muziki wake wa Mugithi na haoni sababu ya kuadhibiwa kwa kuonyesha furaha na burudani. Hata hivyo, NPS imesisitiza kuwa maafisa wa polisi wanawajibika kudumisha nidhamu na taswira ya heshima, hata wanapokuwa nje ya kazi, na kwamba utii wa kanuni za huduma ni wa lazima kwa wote. Samidoh, ambaye amejizolea umaarufu kwa kuunganisha taaluma ya uaskari na muziki, bado hajazungumzia rasmi tukio hilo. Huku uchunguzi ukiendelea, mashabiki wake wanasubiri kwa hamu kuona iwapo atapewa onyo, kuhamishwa, au hatimaye kuachishwa kazi.

Read More