Nviiri The Storyteller Aunga Mkono Marufuku ya Matangazo ya Pombe
Msanii Nviiri The Storyteller ameunga mkono pendekezo la Mamlaka ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) kuwapiga marufuku wasanii na watu maarufu kutangaza bidhaa za pombe. Kupitia ujumbe wake kwa umma, Nviiri amefichua kuwa aliwahi kushiriki kampeni ya matangazo ya pombe mtaani Kayole Jijini Nairobi, lakini baadaye alijutia uamuzi wake huo baada ya kugundua kuwa wakazi wa eneo hilo walihitaji zaidi chakula na fursa za maendeleo badala ya bidhaa za vileo. “Nilijihisi vibaya sana baadaye. Niliona wazi kuwa kile watu wale walihitaji si kileo, bali tumaini na njia za kujikwamua kimaisha,” alisema Nviiri. Msanii huyo ametoa wito kwa wasanii wenzake kuacha kufuata pesa kwa gharama ya maisha ya mashabiki wao, na badala yake kutumia ushawishi wao kwa njia inayojenga jamii. “Tuache kupotosha mashabiki wetu kwa matangazo yanayohatarisha afya na mustakabali wao. Tuna nguvu ya kushawishi na tuitumie kwa busara,” alisisitiza. Kauli ya Nviiri inakuja wakati NACADA ikisisitiza msimamo wake kuhusu athari za matangazo ya pombe yanayohusisha watu mashuhuri, ikisema kuwa yamechangia ongezeko la matumizi ya pombe miongoni mwa vijana.
Read More