Ousmane Dembélé Ashinda Ballon d’Or kwa Mara ya Kwanza

Ousmane Dembélé Ashinda Ballon d’Or kwa Mara ya Kwanza

Mchezaji wa klabu ya Paris Saint-Germain (PSG), Ousmane Dembélé, ameibuka mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka, na kujiunga na orodha ya wanasoka wakubwa duniani waliowahi kushinda tuzo hiyo ya heshima. Dembélé, mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa mwenye umri wa miaka 28, aling’ara msimu uliopita kwa kufunga mabao 35 na kutoa asisti 14 katika mechi 53, akiisaidia PSG kushinda mataji matatu makubwa, likiwemo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo. Katika Ligue 1, Dembélé alikuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 21, hali iliyomfanya ateuliwe kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Ufaransa na pia Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Licha ya mafanikio hayo, pia aliiongoza PSG hadi fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu, ambapo walipoteza kwa Chelsea kwenye mechi iliyochezwa jijini New Jersey, Marekani. Kwa upande wa soka la wanawake, Aitana Bonmatí, kiungo wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, ameweka historia ya kipekee kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon d’Or mara tatu mfululizo. Bonmatí amekuwa na msimu wa mafanikio makubwa na ameendelea kudhihirisha kiwango cha juu cha ubora kwenye uwanja wa soka. Ushindi wa Dembélé na Bonmatí katika toleo hili la tuzo za Ballon d’Or unaashiria mabadiliko ya kizazi katika soka la kimataifa, na pia kuonesha kuwa vipaji vipya vinaibuka na kuvunja rekodi zilizowekwa na nyota waliotangulia.

Read More