Msanii wa Gengetone nchini Kenya, Parroty Vunulu, ameomba radhi kwa mashabiki na umma baada ya kutotimiza ahadi yake ya kunyoa rasta zake iwapo klabu ya Manchester United ingepoteza mechi dhidi ya Tottenham Hotspur. Parroty, ambaye alikuwa ameapa kunyoa dreadlocks zake alizozilea kwa miaka tisa endapo United wangeshindwa, amebadili msimamo wake na kusema hawezi kupoteza utambulisho wake kwa sababu ya matokeo ya mpira. “Heri niache kusupport Manchester United lakini nisipoteze image yangu,” alisema Parroty katika ujumbe aliouweka mitandaoni, akichanganya ucheshi na ukweli kuhusu uamuzi wake wa kutokata nywele hizo. Akiendelea kueleza sababu za kubadili uamuzi wake, Parroty alisema kuwa dreadlocks hizo ni sehemu muhimu ya chapa yake ya kisanii na kimtindo, na kwamba kunyoa nywele hizo kungemgharimu shughuli nyingi za kibiashara. “Nawaomba mashabiki wanielewe. Hizi rasta ndizo zimenitambulisha kwenye game, na kwa kweli zimenisaidia sana kibiashara. Nikizikata, ni kama najifuta kwenye ramani ya muziki,” aliongeza Parroty. Msanii huyo pia alifichua kuwa ana mpango wa kuandaa sherehe maalum ya kusherehekea miaka tisa ya kulea dreadlocks zake mwezi Septemba, kama njia ya kutambua safari yake ya kipekee ya mitindo ya nywele na kujieleza kisanii. “Niko na plan ya birthday kali Septemba. Sitaki tu kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa, bali pia juhudi za kulea hizi rasta kwa miaka yote hii,” alisema kwa msisimko. Wakati baadhi ya mashabiki walichukulia hali hiyo kwa utani, wengine walimkumbusha umuhimu wa kushikilia ahadi. Hata hivyo, wengi walionekana kuelewa msimamo wake, wakitambua umuhimu wa muonekano katika kazi yake ya sanaa. Parroty Vunulu anaendelea kuwa mmoja wa wasanii wa Gengetone wanaovutia kutokana na ubunifu, ucheshi na uaminifu kwa mtindo wake wa maisha.
Read More