Kenya Yatarajia Kung’aa Katika Mbio za Cape Town Jumapili Hii

Kenya Yatarajia Kung’aa Katika Mbio za Cape Town Jumapili Hii

Timu ya wanariadha mashuhuri wa Kenya imepata dhamira mpya kuelekea mbio za marathoni za mwaka huu za Sanlam Cape Town zitakazofanyika siku ya Jumapili. Mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia wakimbiaji wa viwango vya juu kutoka mataifa mbalimbali, huku Kenya ikitarajiwa kung’aa kupitia kikosi chake cha wazoefu na chipukizi. Kwa mujibu wa waandaaji, mbio za wanaume zitajumuisha wakimbiaji wawili walioandikisha muda wa chini ya saa mbili na dakika tano, wanne walio chini ya saa mbili na dakika sita, na wengine wanne walio chini ya saa mbili na dakika saba, ishara ya ushindani wa hali ya juu utakaoshuhudiwa mjini Cape Town. Kwa upande wa wanawake, kutakuwa na wanariadha wawili waliowahi kukimbia kwa muda wa saa mbili na dakika 16 na wengine wawili waliotimiza muda wa saa mbili na dakika 19, wakionyesha ubora wa safu ya wakimbiaji watakaowania taji hilo mwaka huu. Timu ya wanariadha wa Kenya waliodhaminiwa na kampuni ya Sanlam ilikabidhiwa rasmi bendera ya taifa katika hafla iliyoongozwa na aliyekuwa kinara wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya, Paul Tergat. Akizungumza wakati wa tukio hilo, Tergat amewatakia wanariadha hao mafanikio mema akisisitiza umuhimu wa nidhamu, ari ya ushindani, na kupeperusha vyema jina la taifa. Kikosi hicho kinajumuisha majina maarufu kama Lilian Jepkorir, Fridah Lodepa, Vincent Ronoh, na Josephat Kipkoech, miongoni mwa wengine. Wote wanatarajiwa kutoa ushindani mkali dhidi ya wakimbiaji kutoka Ethiopia, Afrika Kusini na mataifa mengine ya bara la Afrika na kwingineko.

Read More
 Uchaguzi wa NOC-K Kufanyika Jumatatu Baada ya Kuahirishwa Mara Mbili

Uchaguzi wa NOC-K Kufanyika Jumatatu Baada ya Kuahirishwa Mara Mbili

Uchaguzi wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOC-K) hatimaye umepangwa kufanyika Jumatatu ijayo, baada ya kuahirishwa mara mbili kutokana na sababu mbalimbali. Awali, uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika tarehe 24 Aprili lakini ukasitishwa kutokana na tofauti miongoni mwa mashirikisho manne kuhusu uhalali wa wajumbe wao wa kupiga kura. Jaribio la pili la kuandaa uchaguzi mnamo tarehe 19 Juni nalo lilikwama kufuatia agizo la Mahakama Kuu lililosimamisha mchakato huo kwa muda. Kwa mujibu wa NOC-K, uchaguzi huo sasa ndio ajenda pekee katika Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa kamati hiyo, ambao ulikuwa umepangwa kufanyika leo. Wadau wa michezo nchini wamekuwa wakiusubiri kwa hamu uchaguzi huu, wakitazamia mabadiliko ya kiuongozi yatakayosaidia kuinua hadhi ya michezo nchini hasa kuelekea mashindano ya Olimpiki yajayo. Kiti cha Urais katika uchaguzi huo kinatarajiwa kushuhudia ushindani mkali kati ya Naibu wa Kwanza wa mwenyekiti Shadrack Maluki na Katibu Mkuu anayeondoka, Francis Mutuku. Wawili hao ni viongozi wa muda mrefu ndani ya NOC-K na wanapigiwa upatu kutokana na tajriba na ushawishi wao katika sekta ya michezo. Jumla ya wapiga kura 29 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo wakiwemo mashirikisho 25 ya michezo, mwenyekiti wa sasa Paul Tergat, wawakilishi wawili wa wanamichezo na mwakilishi wa wanawake. Matokeo ya uchaguzi huu yanatazamiwa kuwa na athari kubwa katika mwelekeo wa kamati hiyo na ustawi wa michezo nchini kwa miaka ijayo

Read More