Msanii Petra Aolewa Na Mr. Hamza Katika Harusi ya Kuvutia
Msanii wa muziki wa rap kutoka Kenya, Petra, ameanza rasmi maisha mapya ya ndoa baada ya kufunga pingu za maisha na mpenzi wake Bw. Hamza katika sherehe ya kifahari iliyofanyika tarehe 14 Septemba 2025 Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Petra alitangaza habari hiyo njema kwa mashabiki wake akipakia picha za harusi na ujumbe wa kugusa moyo uliodhihirisha imani yake kwa Mungu. Alieleza kuwa yeye na mume wake waliombeana mbele za Mungu, na hatimaye wakabarikiwa kuunganishwa kama mume na mke kama ilivyo katika Mathayo 18:19. Katika ujumbe wake, Petra alifafanua pia maana ya jina la Kiebrania Hamza, ambalo tafsiri yake ni “mkono wa ulinzi” unaohusishwa na Jicho la Mungu, ishara ya baraka na kinga ya kiungu. Alisema kwao, jina la Bwana na Bi Hamza ni zaidi ya cheo cha kifamilia, bali ni alama ya agano takatifu lililotiwa muhuri wa ulinzi wa Mungu. Aidha, alimalizia kwa kumshukuru Mungu Mwenyezi, Bwana Yesu Kristo na Roho Mtakatifu kwa kuwa msingi wa ndoa yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ushuhuda wa neema na utukufu wa Mungu. Tangazo hilo liliibua wimbi la pongezi kutoka kwa mashabiki na wasanii wenzake waliompongeza kwa kuanza ukurasa mpya wa maisha yake kama Bi. Hamza. Harusi hii imekuwa hatua muhimu kwa Petra, ikionyesha sura mpya si tu katika maisha yake ya kifamilia, bali pia katika safari yake ya kiroho na kisanii
Read More