Ziara ya Msanii Bad Bunny Kutoa Ajira 8,000

Ziara ya Msanii Bad Bunny Kutoa Ajira 8,000

Mwanamuziki kutoka Puerto Rico, Bad Bunny, ameanza rasmi ziara yake kubwa jijini San Juan nchini Puerto Rico iitwayo “I Don’t Want To Leave” kama njia ya kurudi nyumbani na kuwashukuru mashabiki wake. Ziara hiyo ilianza Julai 11, 2025, na inatarajiwa kukamilika Septemba 14, 2025, ikiwa na jumla ya maonesho 30, yote yakifanyika katika ukumbi maarufu wa José Miguel Agrelot Coliseum Arena jijini San Juan. Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, tamasha hilo linatarajiwa kuvutia mashabiki takribani 600,000 kutoka ndani na nje ya Puerto Rico, hali inayotajwa kuwa kichocheo kikubwa kwa sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla. Taarifa rasmi zinaonesha kuwa ziara hiyo inaweza kuingizia zaidi ya dola milioni 300, sambamba na kuzalisha zaidi ya ajira 8,000, hasa katika maeneo ya hoteli, migahawa, usafiri wa anga na huduma nyingine za kibiashara. Bad Bunny, ambaye kwa sasa anahesabika kama mmoja wa wasanii wenye ushawishi mkubwa duniani, amesema kuwa mbali na kuwapa burudani mashabiki wake, anataka kutumia muziki wake kama daraja la kuinua uchumi wa nyumbani. Ziara hii inatajwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika historia ya visiwa vya Puerto Rico, na inatarajiwa kuacha alama ya kudumu kwenye sekta ya burudani na uchumi kwa ujumla.

Read More