DCCAK Yamkemea Rigathi Gachagua kwa Kutaka Wasanii wa Mlima Kenya Wasusiwe
Chama cha Watayarishaji wa Maudhui ya Kidijitali Kenya (DCCAK) kimemkosoa vikali Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kufuatia wito wake wa kususia wasanii wa eneo la Mlima Kenya waliokutana na Naibu Rais Kithure Kindiki. Kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, DCCAK ilieleza kuwa matamshi ya Gachagua ni ya kurudisha nyuma taifa na ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya uhuru wa kujieleza, ubunifu, na biashara huru. “Tunapinga kwa kauli moja jaribio lolote la kuwanyamazisha wasanii kwa sababu ya maamuzi yao ya kibinafsi ya kisiasa. Huu ni ukiukaji wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo. Chama hicho kilisisitiza kuwa siasa haitakiwi kuwa kizuizi kwa maendeleo ya sekta ya burudani, na kuonya dhidi ya tabia ya kuwatisha wanamuziki na watayarishaji wa maudhui kwa misingi ya misimamo yao ya kijamii au kisiasa. Kauli ya DCCAK imekuja saa chache baada ya video kusambaa mtandaoni ikimuonesha Gachagua akiwashutumu wasanii waliokutana na Kindiki, akiwataka wakazi wa Mlima Kenya kuwasusia. Tukio hilo limezua mjadala mkali mitandaoni, huku wadau wengi wakimtaka Gachagua kuheshimu uhuru wa wasanii na kuacha kuingiza siasa katika masuala ya ubunifu.
Read More